Samba nalicheza haswa lakini jamaa hatosheki, ninapofeli wapi?

Nimeolewa huu mwaka wa nne, najisifu si haba samba nalicheza na ninalijua, lakini mwenzangu hatosheki kiasi naelekea kushindwa.

Nifanyeje?

Umesema samba unaliweza mbona unalalamika kushindwa tena?

Pambana usikubali kushindwa, huu mchezo hauna kuacha ni kuongeza manjonjo.

Fanya hivi ili asikuchoshe. Kwa sababu samba unalijua tumia nafasi hiyo kumchosha mapema kwa kumshika maeneo unayoamini ukiyashika hapindui lazima akubali muziki wako fasta.

Anaweza kukukataza. Jitoe fahamu na ujifanye kama hujamshika maeneo hayo upati kile mlichokusudia, akikuuliza mchezo huo umeanza lini...Mwambie kwa kujiamini umeanza leo (Kwa sauti ya utulivu na ulimi uliolainika).

Usiniangushe, mwanajeshi hodari huwa wa mwisho kusalimu amri.

Shemeji zangu wakali kuliko mke wangu, wananitoa udenda

Anti habari!

Samahani kwa hili nilisemalo, napata wakati mgumu mke wangu analeta ndugu zake wakali kuliko yeye na wana mitego kiasi kwamba ninaingia majaribuni.

Nifanyeje?

Acha tamaa, umeziendekeza ndiyo maana zinakupeleka puta.

Kama mkeo ni mwelewa mwambie kinaga ubaga kuhusu tatizo lako dhidi ya hao ndugu zake, akiwa na nia ya kunusuru ndoa yake atakusikia. Lakini akiichukulia kwa mtizamo hasi hiyo kauli yako utazua utata mpya.

Ukishindwa kumueleza kuwa unapata matamanio awaondoe mweleze wabadili aina za mavazi kwa sababu hayana maadili, labda wakijistiri kidogo itasaidia kuondoa tatizo ulilonalo.

Ila muombe sana Mungu akuondolee jinamizi baya ulilonalo. Hivi ukijua tu huyu ni shemeji yako si inatosha kuwa na nidhamu unapomuona.

Mthamini mkeo, kuwaona wadogo zake wakali kuliko yeye ni kumdharau.

Sielewi anataka nini

Mume wangu nahisi ananitafutia sababu, kwa kuwa nikivaa suruali hataki, na nikivaa gauni anasema sijapendeza, siku nikivaa nguo za vitenge anasema eti nimezeeka, nikisuka nakosea, nikisema leo nichane hataki, Anti kwa kweli sijui huyu mtu anataka nini hasa?

Jibu: Fanya hivi kwa muda wa mwezi mmoja, mwambie akupangie nguo za kuvaa anazopenda yeye ili uone chaguo lake ni nini.

Siku nyingine muulize kijanja “Mume wangu unapenda mwanamke avae nguo za aina gani, au mwanamke anayekuvutia ni anayevaa nguo za aina gani” jibu atakalokupa utajua anachokitaka.

Ila usijibane sana wakati mwingine ni bora kufanya kile kinachokupa raha ilimradi hakivunji sheria na kukutoa utu wako mbele ya jamii.