Serikali kuchunguza orodha tata ya vitambulisho vya RC Iringa

Thursday May 30 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati waandishi wa habari mkoani Iringa wakitoa siku saba kwa mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi kuwaomba radhi kwa madai ya kuwataka kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali, Serikali imesema inafuatilia suala hilo.

Desemba 10, mwaka jana, wakati Rais John Magufuli akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alianzisha utaratibu wa kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo ambao mauzo yao ghafi hayazidi Sh4 milioni kwa mwaka.

Wakuu wa mikoa wote nchini walikabidhiwa vitambulisho hivyo na kutakiwa kuvitoa kwa wafanyabiashara hao kwa Sh Sh20,000.

Rais alisisitiza kuwa mfanyabiashara atakayekutwa na kitambulisho hicho asisumbuliwe katika shughuli zake na mamlaka yoyote ya kukusanya kodi na ushuru.

Lakini hivi karibuni, mkuu wa mkoa wa Iringa, Ali Hapi alitoa orodha ya makundi 47 ya watu kulingana na shughuli zao, ambao wanatakiwa kuwa na vitambulisho hivyo hadi ifikapo Juni 17, mwaka huu.

Hata hivyo, baada ya orodha hiyo kutoka, maswali yaliyojaa utata bila majibu yaliibuka, wapo waliojiuliza kama mkoa huo ulipewa maelekezo tofauti na mikoa mingine.

Advertisement

Miongoni mwa makundi yaliyotajwa na Hapi kuwa yanastahili kuwa na vitambulisho hivyo na kuibua maswali ni waandishi wa habari, vibarua wa viwandani wasio na mikataba maalumu, wanachama wote wa saccos za Iringa, wafanyakazi wote wa supermarket, vituo vya mafuta, nyumba za wageni, migahawa, baa na wafugaji wa nyuki.

Wengine ni waliowezeshwa na mfuko wa Tasaf na waliopiga hatua kwa msaada huo, wanachama wa vikundi vya vicoba, madereva wa daladala, bodaboda, mabasi, hiace, walio kwenye sekta ya utalii, wakusanya mazao na wanaokopi na kurekodi nyimbo.

Jana, Mwananchi lilimtafuta naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara ili kupata ufafanuzi wa orodha hiyo ya mkuu wa mkoa ambaye alisema analifanyia kazi jambo hilo na ametuma watu walifuatilie.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), jana lilitoa tamko kuelezea masikitiko yake juu ya maagizo hayo yaliyotolewa na kiongozi huyo kwa waandishi wa habari kuwa nao wanapaswa kuwa na kitambulisho hicho cha ujasiriamali.

“TEF imesikitishwa zaidi na kauli ya Ndugu Hapi kuwa amefikia uamuzi huo kuhakikisha kila mtu analipa kodi, ifahamike kuwa mkuu wa mkoa hana mamlaka ya kutoza mtu kodi. Chombo pekee chenye mamlaka ya kutoza kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ikiwa nia yake katika vitambulisho ni kulipisha kodi, basi amerejesha kodi ya kichwa iliyofutwa mwaka 2004,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.

Alisema waandishi wa habari waliotajwa kwenye orodha hiyo namba 36, hawana bidhaa wanazouza, hivyo agizo la Hapi anatindikiwa uelewa wa sheria za nchi, hakuomba ushauri wa kisheria au amejielekeza vibaya.

Balile alisema kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (MSA 2016) na kanuni zake za mwaka 2017, kinatambua taaluma ya uandishi wa habari na waandishi wa habari.

Alisema kazi za waandishi wa habari ni kukusanya, kuchakata, kuhariri na kuchapisha habari na taarifa na iliweka utaratibu wa kulipia vitambulisho vya kazi (press card) Sh30,000 kila mwaka.

“Tungependa kumkumbusha Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuwa waandishi wa habari wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na si kupitia maagizo na matamko. Tunaamini kwa maelezo haya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa atatambua kwamba amejielekeza vibaya katika agizo lake la kuwataka waandishi wa habari wakanunue vitambulisho vya watu wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi,” alisema Balile.

Hata hivyo, ufafanuzi wa awali wa Hapi katika mitandao ya kijamii, alieleeza kuwa waandishi wa habari waliolengwa ni wale wasio na mikataba ya ajira katika vyombo vyao, lakini baadaye alitoa ufafanuzi mwingine kuwa waandishi wa habari, madereva bodaboda na bajaji hawahusiki.

Jana, waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa walimpa siku saba Hapi awaombe radhi.

Advertisement