Shahidi aeleza alivyozimia kwenye maandamano

Thursday May 16 2019

Mwenyekiti wa Chadema, freeman Mbowe (kushoto0

Mwenyekiti wa Chadema, freeman Mbowe (kushoto0 akijadiliana jambo na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko  kabla yakunza kusikilizwa kwa kesi inayowakabili wao na viongozi wengine wachama hicho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wanane ameeleza jinsi alivyozimia siku ya tukio.

Shahidi huyo, E 6976 Koplo Rahimu Msangi alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Wankyo Simoni, Koplo Msangi alidai kuwa mkuu wa operesheni Mkoa wa Kinondoni, Gerald Ngichi alitoa amri ya kupiga mabomu ili kutawanya waandamanaji.

Alidai kuwa baada ya kufyatua mabomu, upepo ulikuwa ukielekea walipo polisi na alishtukia amepigwa jiwe na kujikuta amepoteza fahamu akiwa yuko hospitali ya polisi, Barabara ya Kilwa.

Alidai baada ya kupata kumbukumbu alikumbuka alikuwa na silaha aina ya SMG na aligundua haioni akiwa ametundikiwa dripu. Alidai Februari 17, 2018 alifika Afande Mzelengi na kumuuliza alikuwa na silaha lakini hafahamu iko wapi na kumueleza iko Kituo cha Polisi Oysterbay.

Koplo Msangi alileleza akiwa hospital aligundua alikuwa ameumia kwenye maandamano baada ya kupigwa jiwe upande wa kulia wa shingo na kudai kuwa alimshuhudia Mbowe akihamasisha maandamano kuelekea kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

Alidai kuwa Februari 16, 2018 alifika kazini saa 12 asubuhi na kupangiwa kufanya doria Wilaya ya Kinondoni akiwa na wenzake sita na siku hiyo saa 11:00 jioni wakiwa Barabara ya Mwenge, ITV iliingia simu ya upepo kutoka kwa OCD Dotto na kumpa maelekezo askari Mohammed Selengi kuelekea viwanja buibui Mwananyamala.

Alidai kuwa walielezwa katika viwanja hivyo kulikuwa na mkutano wa Chadema unaoendelea na kuna viongozi waliokuwa wanatoa maneno ya uvunjifu wa amani wakiwa jukwaani.

Alidai kuwa alipofika, alimshuhudia Mbowe akichukua kipaza sauti kutoka kwa mgombea (ubunge wa Kinondoni, Salum Mwalimu) na kutoa tamko la kuwasindikiza viongozi waliokuwa eneo hilo kwenda kwa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kuchukua barua zao na kisha kushuka kwenye jukwaa na wananchi waliokuwa kwenye uwanja huo walikuwa na hasira zilizosababishwa na viongozi akiwamo Mbowe.

Alidai kuwa wananchi walitaharuki na kutoa kauli za uvunjifu wa amani kwa kusema hatuogopi, hatutishiki tutaandamana hadi kieleweke.

Alidai kuwa afande Mselengi aliitwa kwa simu ya upepo na kuambiwa aelekee Mkwajuni maandamano yanaendelea na walipita barabara za pembezoni na walipofika hapo walimkuta mkuu wa operesheni wa mkoa afande Ngichi.

Alidai kuwa walipofika, waliamriwa kushuka kwenye magari wakati huo maandamano yakiendelea huku waandamanaji wakisema hatuogopi mtatuua wakiwa wamebeba mawe, chupa na wengine wamejifunika nyuso.

Alidai kuwa afande Ngichi alitoa ilani ya kuwataka kutawanyika lakini hawakutaka kusitisha maandamano.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 31 mwaka huu kwaajili ya kuendelea na ushahidi kwa upande wa Mashtaka.

Advertisement