Siasa ilivyowatibua nyongo mashabiki wa Taifa Stars Afcon

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imemaliza mechi zake tatu katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) inayoendelea nchini Misri.

Taifa Stars imecheza mechi tatu katika kundi lake la C ambalo pia lilikuwa na timu za Kenya, Senegal na Algeria.

Katika kundi hilo Senegal na Algeria zimefanikiwa kufuzu hatua ya mtoano na kuungana na timu zilizofanikiwa kupita hatua hiyo kutoka makundi mengine kwenye michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza imeshirikisha timu 24.

Mechi tatu ilizocheza Satars katika michuabo hiyo imepoteza zote ilianza kufungwa na Senegal katika mechi yake ya kwanza ilipolala kwa magoli mawili kwa bila kisha kufungwa na Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ magoli 2-3 na mwisho ikapoteza mbele ya Algeria juzi, ilipolala 2-0.

Yawezekana yapo mengi yaliyochangia Taifa Stars kupoteza michezo yake yote kwenye michuano hiyo ambayo Tanzania imeshiriki kwa mara ya pili baada ya kupita miaka 39, lakini kuingizwa siasa ni miongoni mwa mambo yaliyowafanya Watanzania watumbukie nyongo na kuwagawa mashabiki kimtazamo.

Kauli ya kiongozi kijana

Katika hatua zote za maandalizi Watanzania walisimama pamoja na kuiunga mkono kwa hali na mali kusaka mafanikio kwenye michuano hiyo, ingawa ilifahamika kuwa sio kazi rahisi kuvuka japo hatua ya awali kutokana na ukweli kuwa Afcon inavikutanisha vigogo vya soka Afrika. Hata hivyo, kila mmoja alitanguliza uzalendo na kuiombea mafanikio.

Hata hivyo, baadae kulianza kuonekana kuingizwa siasa tena zile zenye kuwagawa wapenzi kwa timu yao baada ya ‘kiongozi kijana’ kuyanasibisha mafanikio ya timu hiyo na chama chake cha siasa, hivyo kuwatoa katika mstari baadhi ya watu hususani wale wanaoamini tofati katika kile ambacho kiongozi huyo anakiunga mkono. Kiongozi huyo katika kauli yake iliyowanyong’onyesha baadhi ya mashabiki wa Taifa Stars alisema timu hiyo ni ya Serikali, hivyo inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba itashinda kama ambavyo CCM imekuwa ikishinda.

Mbali na kauli hiyo, katika kile kilichoonesha Stars imeingizwa kwenye siasa ni kauli nyingine ya kiongozi kijana akikosoa baadhi ya maoni na mtazamo wa wabunge kuhusiana na timu hiyo baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Senegal.

Mbele ya Rais John Magufuli, Juni 25 mwaka huu, alisema ameumizwa na baadhi ya watu wanaotoa maoni na kuwabeza wachezaji wa Taifa Stars.

Siku chache kabla ya kauli yake kundi la wabunge 50 walioongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai lilirejea nchini kutoka Misri walikokwenda kuongeza hamasa na ushangiliaji wakati wa mechi dhidi ya Senegal ambapo walisema wamebaini mambo kadhaa yaliyosababisha Tanzania ishindwe mechi hiyo.

Kiongozi kijana akasema. “Nimeumizwa na matokeo ya Taifa Stars, lakini nimeumizwa zaidi kwa watu kuwabeza wachezaji wetu ambao wametubeba Watanzania ambao ndani ya miaka 30, haikuwezekana lakini wao wamepambana mpaka tupo Afcon leo hii.”

Juni 25, mwaka huu akijibu mwongozo ulioombwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) aliyehoji kauli iliyotolewa na kiongozi mmoja wa Serikali, akidai kuwa inalidhalilisha Bunge, Ndugai alisema, “Hayo ni mawazo ya mtu ambaye kidogo ndio hivyo. Ni bahati mbaya sana tuna viongozi wa Serikali wanadiriki kumdanganya Rais hadharani, kiongozi wa Serikali unapoongea mbele ya rais jipange ongea ukweli mtupu wa mwenyezi Mungu, usisingizie wala kumuonea mtu hatufanyi hivyo.” Kauli za wanasiasa na majibizano yao kuhusu Taifa Stars hususani katika kipindi muhimu cha ushiriki wa fainali za Afcon, ziliwagawa Watanzania na mashabiki kwa kuwaondoa kwenye hoja ya mpira na kuwaingizia siasa jambo ambalo halikuwa na afya kwa soka.

Wabunge na safari Cairo

Baadhi ya wabunge waliokwenda Misri kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuhamasisha ushindi waliporejea kila mmoja alisema lake juu ya kile walichoamini kimechangia kushindwa kwa Taifa Stars.

Mbunge wa kuteuliwa Abdallah Bulembo, alitoa lawama kwa Kocha Mkuu Emmanuel Amunike akidai anastahili kubeba lawama za Taifa Stars kufungwa.

Bulembo alidai kushangazwa na kitendo cha Amunike katika mechi ya Taifa Stars dhidi ya Senegal kumpanga John Bocco acheze winga badala ya mshambuliaji wa kati hatua iliyompa wakati mgumu mshambuliaji mahiri wa Stras, Mbwana Samatta kucheza kwa ufanisi.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia naye alitupa lawama kwa kocha huyo akitilia shaka uhodari na uwezo wa Amunike katika kuivusha Tanzania kwenye michuano hiyo.

“Kocha wa timu ya Taifa ana rekodi gani hadi apewe timu. Nilikaa na rais wa chama cha soka cha Nigeria, alisema kama angepata nafasi ya kutupa ushauri angetuambia yule sio kocha, lakini pamoja na yote Tanzania inabidi tuwekeze kwenye timu ya Taifa,” alisema.

Maoni ya wabunge hao yaliegemea katika kumlaumu mwalimu wa timu huyo ambaye tangu amekabidhiwa mikoba ya kuinoa Taifa Stars sasa ni miezi 11.

Hata hivyo, Amunike alisema ataendelea kusimamia taaluma yake na hawezi kuharibu kazi yake kwa sababu ya cheo au nafasi ya mtu. “Nimeona lazima niseme naona kila mmoja anajua mpira nitaendelea kufanya kazi yangu na siwezi kuharibu taaluma yangu kwa cheo cha mtu wala fedha alizonazo lakini ninachojua ni kuheshimu watu wote uwe mdogo, masikini na hata tajiri,” alisema.

Mtazamo wa wadau

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Mkwasa anasema si wakati mwafaka wa kumlaumu kocha Amunike.

“Tumpe muda, pamoja na kufungwa lakini tumepambana. Taifa Stars kuifunga Senegal ingekuwa jambo kubwa,” alisema Mkwasa.

Mchambuzi Ally Mayay anasema baada ya matokeo ya hatua ya makundi wadau wanatakiwa kuangalia kasoro za Taifa Stars. “Ukiangalia Senegal walipiga mashuti 21 na kufunga mara mbili, maana yake ni nini, tulipambana. Katika mechi yenye ‘shoot on target’ 21 kisha tunafungwa mbili hapo unamlaumu vipi kocha,” alisema Mayay.

Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Idd Kipingu alisema ni mapema kumtwisha lawama Amunike. “Ni kweli tunahitaji mafanikio, lakini si hivyo tunavyofikiria tumpe kocha muda,” alisema Kipingu akitoa maoni baada ya mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Senegal.

Huu ndio ukweli

Ushindi na uimara wa timu yoyote katika soka unatokana na uwekezaji unaofanyika katika kujenga misingi ya kisoka kama kuwa ligi bora na timu za vijana.

Katika nchi zilizoendelea kisoka kama Uingereza, Hispania au Ujerumani jukumu la maendeleo ya soka linaachwa kwa chombo kilichopewa mamlaka hayo, viongozi wa siasa na wadau wengine kama wanao mchango wowote hasa wa kiushauri wanaweza kuuwasilisha katika chombo hicho hali ambayo kwa Tanzania imeshuhudiwa kuwa tofauti.

Wanasiasa waliamua kuingia katikati ya soka na kulitumia kuwa kama jukwaa la kutunishiana misuli hatua ambayo haiwezi kuachwa kunyooshewa vidole wakati huu tunaposubiri kuwapokea vijana wetu wanaorejea nchini baada ya kupoteza michezo yote mitatu.