TCRA yatoa neno kwa watumiaji wa mitandao

Friday March 15 2019

By Yonathan Kossam, Mwananchi. [email protected]

Mbeya. Watumiaji wa huduma za mawasiliano Tanzania wametakiwa kutambua wanayo haki ya kupata huduma sahihi pamoja na kutumia vyombo salama vya mawasiliano.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Machi 15, 2019 na Mchumi Mwandamizi Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Godliving Kessy jijini Mbeya katika maadhimisho ya siku ya haki za watumiaji huduma za mawasiliano duniani ambayo huadhimishwa Machi 15 kila mwaka.

Kessy amesema vifaa janja kila siku vinaongezeka na kama si salama kwa watumiaji vinaweza kuleta madhara ikiwemo kutopata huduma inayofaa.

"Tunaungana na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuhakikisha watumiaji wanatambua haki zao pamoja na wajibu wao pia," amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda TCRA, Nyanda za Juu Kusini, Asajile John amesema watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini watumie vizuri fursa ya kulalamika badala ya kunung'unika pale wanapopata huduma isiyofaa.

Makamu Mkuu wa Shule ya Ufundi na Sayansi Iyunga ambapo maadhimisho hayo yamefanyika Imani Mwambene, ameishukuru mamlaka hiyo kwa kupeleka elimu kwa wanafunzi hao kwani itakuwa msaada kwa Taifa siku za usoni.

 

Advertisement