Tohara ilivyomponza mtoto hadi kukatwa miguu yote

Thursday January 24 2019

Madaktari wamkimfanyia tohara  mkazi wa Katoro

Madaktari wamkimfanyia tohara  mkazi wa Katoro mkoani Geita katika kituo cha Katoro,jana wakati Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na Afya ya IntraHealth inatoa huduma hiyo bila malipo. Picha na Michael Jamson 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Matumaini mapya ya mtoto Chistopher Masaka (11) ambaye alikatwa miguu yote mwishoni mwa mwaka jana baada ya kufanyiwa tohara mwaka 2017 yameanza kurejea.

Christopher, mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mtitaa, alikatwa miguu yote kutokana na ushauri wa madaktari wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Akizungumzia mkasa huo baba mzazi wa mtoto huyo, Elias Masaka wa Kijiji cha Mtitaa, Bahi alisema Christopher alizaliwa akiwa mzima kabisa.

Mara baada ya kutahiriwa na ngariba, kijana huyo alianza kuugua miguu akisema alikuwa akihisi kama kuwa vitu vilivyokuwa vikitembelea kwenye nyayo zake.

Baba huyo alisema kadri muda ulivyosonga, tatizo hilo liliendelea na kufikia hatua ya kuanza kutoa majimaji.

Alisema hata aliporejeshwa kutoka jandoni haikuwezekana tena kupelekwa shule kwani wakati huo alikuwa hawezi kutembea umbali mrefu.

Mzazi huyo alisema hakuwahi kukutana na tatizo kama hilo katika ukoo wao wala katika kijiji chao lakini akasema wanajiuliza ni kwa nini chanzo cha tatizo hilo kianzie wakati wa tohara.

Wakati mtoto huyo akisema kwamba hajawahi kuambiwa chanzo cha maradhi yaliyomsibu, Mkurugenzi wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika alisema tatizo alilokuwa nalo mtoto huyo lilikuwa kubwa ambalo bila ya kumkata miguu isingewezekana kumsaidia.

“Magonjwa kama haya yanakuwa na historia yake, lakini siwezi kuingia ndani zaidi ila ninyi mtambue kuwa tumemsaidia kama hospitali kwa kushirikiana na mheshimiwa Anthony Mavunde na hapa tumeshaokoa uhai wake,” alisema Dk Chandika

Christopher ambaye jana aliripoti katika Shule ya Fountain Gate Academy jijini Dodoma kuendelea na masomo ya darasa la pili, alisema ndoto yake ilikuwa imekufa baada ya kukatwa miguu lakini anaona tumaini jipya kwani anataka kusoma na kuwa mwalimu mzuri siku za usoni.

“Sema hapa shida yangu itakuwa ni Kiingereza ambacho wanazungumza wenzangu maana sijui, lakini kwa vyovyote nitajitahidi hadi nijue na tuweze kuwa pamoja na mazingira nitayazoea tu,” alisema Christopher.

Christopher amepata ufadhili wa kusoma katika shule hiyo kutoka kwa mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na kuhusu hilo, alimshukuru mbunge huyo kwa kutimiza ndoto yake na kuahidi kusoma kwa bidii ili awe kinara wa darasa lao.

Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana alisema uamuzi wake wa kumsomesha umetokana na kuwa wazazi wa kijana huyo hawana uwezo kumhudumia katika hali ya ulemavu.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji wazazi wa Christopher walikata tamaa na kuona mwisho wa maisha ya mtoto huyu. Leo nimeamua kumkabidhi rasmi hapa shuleni ambapo nitakuja kumtembelea mara kwa mara kuliko angekuwa kule Bahi mbali,” alisema Mavunde.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Japhet Makau alisema wamempokea na kumpa nafasi Christopher ili waweze kutimiza ndoto yake na ni utaratibu wao kusomesha yatima ambao wanakuwa wamekosa wa kuwasaidia.

Alisema hadi sasa wameshakuwa na yatima 20 katika shule hizo zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Advertisement