Tufuatilie maisha ya watu wetu nchi za nje

Zanzibar ilitajwa hivi karibuni kuwa na mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu na kutolewa ushauri wa kuwa na sheria kali zinazodhibiti biashara hii.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa ni kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji (IOM) limegundua kuwepo tatizo hilo Visiwani.

Akitoa taarifa hiyo, Dk Samuel Likindoki aliuambia mkutano uliofanyika Zanzibar hivi karibuni kwamba katika utafiti aliouongoza iligundulika kwamba watu wanaosafirishwa kutoka Zanzibar huahidiwa kufanya kazi zenye maslahi mazuri huko ng’ambo, lakini baada ya kufika huko walikopelekwa hukuta hali ni tafauti.

Hii ni habari ya kusikitisha, lakini kwa bahati mbaya huo utafiti kwa mujibu wa namna ambayo matokeo yake yalivyowasilishwa, hautoi sura halisi ya suala hili kwa vile maswali mengi hayana majibu yake.

Kwa mfano, hapana maelezo ya utafiti huu ulifanywa na watu wangapi, lini na sehemu gani za Visiwani na ni watu wangapi walihojiwa.

Vile haiwekwi bayana hawa wanaosafirishwa hupelekwa nchi gani au hatua gani zimechukuliwa kuwashughulikia wanaofanya biashara hii haramu na kama zimechukuliwa ni hatua zipi na watu wangapi wamewajibishwa kisheria.

Katika ripoti hio tunaambiwa takwimu za dunia zilizofanywa mwaka 2014 (haielezwi na nani) zinaonyesha watu 350,000 walisafirishwa nje ya nchi. Lakini, haielezwi ni kwa mwaka mmoja au zaidi ya hapo.

Vilevile hapana maelezo ya kutosha ya kuonyesha kati ya watu hawa, wangapi walisafirishwa kutoka Bara na wangapi kutoka Visiwani na walikwenda nchi gani.

Katika hali kama hii pia ungetarajiwa kupata angalau dokezo la hatua gani Serikali za Zanzibar na ya Muungano zilichukua kuwasiliana na Serikali za nchi wanakopelekwa hawa watu kufanya kazi kama ‘nusu watumwa’.

Mara nyingi imekuwa ikielezwa umuhimu wa takwimu sahihi na za uhakika na si maelezo ya jumlajumla wakati yanapotolewa maelezo ya suala lenye umuhimu mkubwa kwa maisha ya watu.

Taarifa za jumla jumla huwa hazisaidii na wale wanaotaka kusaidia kufuatilia ili biashara haramu kama hii ikomeshwe, huwa hawajui wapi pa kuanzia.

Ni vizuri kwa taasisi kubwa na zenye kuheshimika kama IMO ambayo tunaambiwa ndiyo iliyofanya utafiti, ikatoa maelezo ya kina na kuonyesha juhudi zilizofanywa za kukabiliana na hali hii mbaya.

Mara nyingi hapa kwetu panapotokea chombo cha habari, hasa cha binafsi, kutoa habari kama hii bila ya maelezo yakinifu tunaona kinapewa adhabu, kama ya kufungiwa na kutolewa maelezo marefu kuonyesha lengo lilikuwa ni kupotosha umma.

Lakini, wanapofanya wengine huonekana sawa na taarifa zisizokuwa na mshiko hutakiwa zipokelewe kwa mikono miwili kama vile hazina dosari.

Wakati umefika kwa masuala nyeti kama hili la biashara haramu ya binadamu yakatolewa maelezo ya kuridhisha na hapo ndipo waandishi wa vyombo vya habari vya hapa nchini na wasamaria wema wanaweza kufuatilia na kuisaidia serikali kupata suluhisho.

Ni vizuri tukajitahidi wakati unafanyika utafiti basi ukawa na wigo mpana na inapowezekana vyombo vya habari vikaelewa juu ya kufanyika kwake, kama si jambo la siri, ili viweze kusaidia utafiti huo kuwa na mafanikio na kufikiwa matarajio ya lengo la kufanyika kwake.

Hapana ubishi kwamba suala la biashara haramu ya binadamu hivi sasa imekithiri duniani na imeleta maafa, ikiwa pamoja na watu kupoteza maisha na wengine, hasa wanawake na watoto kudhalilishwa huko walikokwenda.

Watu hawa huwa hawana mahali pa sauti zao kusikika kwa vile serikali za nchi hizo hujifanya kama hazina taarifa hizo, lakini bado huwa tunaziangalia kama nchi rafiki wakati raia wetu huwa wanateseka katika nchi zao.

Nchi nyingi siku hizi hutumia ofisi za mabalozi wao katika nchi mbalimbali kufuatilia maisha ya raia wa nchi zao katika hizo nchi walizopelekwa kuziwakilisha nchi. Wakati umefika kwa ofisi zetu za mabalozi nazo kulishughulikia suala hili.

Tusiruhusu urafiki wetu na nchi za nje kufumbia macho madhila wanayofanyiwa watu wetu katika nchi hizo.

Tanzania tunayo rekodi nzuri ya kuwatendea utu na ubinadamu raia wa nje kama tunavyowafanyia wananchi wetu. Nasi tuhakikishe Watanzania waliopo nje, nao wanaheshimiwa utu wao, hasa na hizo nchi tunazosema ni rafiki wa Tanzania.