Tuna vibaraka wa mabeberu au hizi rafu za kisiasa?

Mabeberu au vibaraka wa mabeberu ni nani? Kwa siku za karibuni haya ni maneno ya kawaida. Ni sehemu ya majibizano yanayoendelea miongoni mwa wanasiasa na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Kwa tafsiri rasmi ya kamusi ya Kiswahili, ubeberu ni mfumo wa kimataifa wa siasa, uchumi wa uzalishaji mali wa kiwango cha juu kabisa cha ubepari ambapo mataifa tajiri huvuka mipaka yake na kwenda kunyonya uchumi wa nchi maskini.

Japokuwa tafsiri hiyo haiwezi kuwa katika muktadha wa kidunia, inapingwa na waumini wa nadharia ya mfumo wa kibepari.

Kumbukumbu zinaeleza kuwa mwasisi wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere kwa wakati huo alikuwa mstari wa mbele kupinga vikali kila chembe ya ubeberu katika ardhi ya Tanganyika na Afrika, akilaani viongozi waliotumiwa na mabeberu kukwamisha harakati za ukombozi.

Mbali na kumbukumbu hiyo, ubeberu umeendelea kuwa vinywani mwa wanasiasa, japokuwa kwa muktadha tofauti.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe hivi karibuni walikuwa miongoni mwa wanaojibizana kuhusu suala la ubeberu.

Ni mchezo wa kisiasa?

Mhadhiri kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja anasema hakuna vibaraka wa mabeberu katika mfumo wa siasa kwa nyakati hizi hapa nchini na vibaraka hao hawawezi kupata nafasi ya kupenyeza ajenda zao katika mageuzi ya kisiasa yaliyokomaa kidemokrasia.

“Hawawezi ku-survive, kwamba wakaleta ajenda yao, wakashirikiana na watu wa nje halafu wakaangusha uchumi na kupeleka mali kutoka Tanzania kwenda nje, sioni kama tunao, ila naona ni neno ubeberu linatumika kama tusi kuwabagua baadhi ya viongozi,” anasema Profesa Semboja.

“Kuna watu wanafikiri wao ndiyo wazalendo kwa wananchi, wana nia ya maendeleo ya wananchi halafu hawa wengine hawana uhusiano na wananchi ila wana uhusiano na watu wa nje, kitu ambacho sikioni katika mfumo wa sasa. Isipokuwa katika siasa inaweza kutokea kuchafuliana.”

Lakini Dk Bashiru, msomi wa Sayansi ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anawazungumzia wanasiasa anaosema wanafanya upotoshaji wa takwimu kila wanapojadili hali ya uchumi wa Taifa ili kuwanufaisha mabeberu wanaowafadhili.

“Tunaweza kutofautiana, ila kupotosha ni dhambi kwa msomi tena aliyesoma UDSM. Najua ugonjwa anaougua, kawekwa mfukoni na mabeberu. Wanamlisha, wanamvalisha, wanamsafirisha, Kavimba kichwa anaanza kupotosha uchumi wa nchi yetu. Hali ya uchumi wetu ni imara,” anasema Dk Bashiru bila kumtaja mwanasiasa huyo.

Anaongeza, “hakuwa hivyo, alikuwa ni kijana anayejenga hoja, na unavutiwa na hoja zake lakini tangu alipoanza kujiita kiongozi mkuu wa vyama kuliko vyote...”

Ingawa hakumtaja, ilionekana dhahiri, Dk Bashiru anamlenga Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye pia anamtaka Dk Bashiru kuendeleza utamaduni wa kujadili masuala na si kujenga tuhuma za ubeberu ambazo hazina ukweli.

“ACT tulisimamia suala la korosho, suala la pensheni za wafanyakazi, haikuwa kweli? Tulisimamia suala la sheria ya waandishi wa habari, je, waandishi hamshughulikiwi?” anahoji mbunge huyo wa Kigoma Mjini

“Kila jambo tunaloshughulikia limekuwa na maslahi ya umma na matokeo yake yanaonekana. Leo CCM wanapata shida na korosho, wangetusikiliza wasingepata shida, kwa hiyo, hivyo ni vihoja tu na ACT tutaendelea kuelimisha umma kwamba serikali imeshindwa kuuendesha uchumi wa nchi yetu,” anasisitiza Zitto akimjibu katibu mkuu wa CCM.

Dalili za vibaraka

Katika mfumo wa siasa za kimataifa, kuna wanamageuzi Afrika walioumizwa na walionufaika na ubeberu. Historia ikimtaja Jonas Savimbi, msomi wa sayansi ya siasa nchini Angola aliyepambana kumng’oa mkoloni lakini baada ya kuikosa Ikulu, aliamua kuingia msituni kuendeleza vita ili aongoze nchi, akipewa silaha na mabeberu waliohitaji shaba na mafuta.

Mbali na Savimbi, waziri mkuu wa kwanza wa Zaire (sasa DRC), Patrice Lumumba alishika nafasi hiyo kwa miezi mitatu kabla ya kuuawa kutokana na misimamo ya kupinga wazi unyonyaji wa kibeberu.

Katika muktadha huo, Dk Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yeye anaamini vibaraka wa ubeberu wanaweza kujitokeza kwa namna moja au nyingine kutokana na sababu kadhaa, kutokana na ushahidi wa vita hiyo ya ubeberu.

Msomi huyo anasema vyama vya siasa, hupata ufadhili wa fedha kutoka nchi za magharibi baada ya kushawishika na mlengo (imani ya chama cha siasa) wa vyama unaohusiana na maslahi yao.

“Wafadhili hao wa vyama hawawezi kutoa fedha kwa vyama hivyo bila kuwa na ajenda zao au wanaweza kukupa fedha kwa sababu unajaribu kufuata mlengo wao wa kisiasa. Ndiyo maana vyama vinapoungana utasikia ni vyama vyenye mlengo unaofanana kwa hiyo wanaweza kuwepo si kwa kuunga mkono mabeberu ila kutokana na mwingiliano huo,” anasema Dk Mbunda.

Dk Mbunda anasema hali hiyo inathibitishwa kwa mifano ya nadharia mbalimbali hususani ya utegemezi unaoendana na ukoloni mamboleo, pamoja na nadharia ya False Paradise inayotumika katika upandikizaji wa elimu za magharibi kwa lengo la kubadili mitazamo ya kijamaa kwenda ubeberu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji anasema ni kweli hakuna chama cha siasa ikiwamo CCM, kisichopatiwa ufadhili wa fedha za kukuza mtandao lakini si kila ufadhili unakuwa na masharti ya kufuata mlengo fulani au kutekeleza ajenda zinazokinzana na maslahi ya Nchi.

Dk Mashinji anasema; “kama kuna mtu anatumia hiyo nafasi ya kuwagawanya watu, kuleta vurugu, tunatakiwa ku-deal naye kwa tatizo analolifanya lakini hatuwezi tukatumia ujumla kulaumu. Kwa Tanzania hatuna watu kama hao kwa sasa katika siasa, labda wako kwenye taasisi nyingine, lakini katika siasa kuna watu wanauza ajenda zao tu, wanaowasingizia wanatafuta kiki wasukume maisha yao mbele.”