Uchaguzi 2020 ni ajenda mbili tu za ushindi- Zitto

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza alipokuwa akihojiwa na waandishi wa Mwananchi Communications Limited, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wapinzani watakuwa na ajenda mbili za kuombea kura kwa wananchi.

Amezitaja ajenda hizo kuwa ni kile alichokiita uminywaji wa haki na hali ya uchumi nchini.

Zitto alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika juzi mjini Dodoma.

Aliulizwa kama atamudu kushinda tena nafasi ya ubunge wa Kigoma Mjini na nafasi ya chama chake katika kinyang’anyiro cha ubunge kwenye majimbo mengine na kiti cha urais wa Muungano na Zanzibar.

Zitto alisema “haki kwa maana ya masuala yote ya uvunjifu wa haki, wapo watakaopiga kura kwa sababu nyavu zao zimechomwa moto, hawa wana ajenda yao kuhusu uvuvi. Hivi utawaeleza nini wakulima wa korosho, mbaazi, tumbaku na kahawa wanavyopitia kipindi kigumu kwa sasa. Bei za mazao hayo zimeporomoka na wana hali mbaya,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini katika mahojiano hayo.

“Hakuna eneo ambalo linawahusu wananchi Serikali haijakosea. Kuna wafanyabiashara wanalia kila siku. Tuna hoja za msingi kwa maana ya masuala ya haki na uchumi. Ajenda haitakuwa ndege maana wanaopanda ni asilimia tano tu.”

“Ajenda haitakuwa reli ya kati maana mpaka wakati huo itakuwa imeishia Morogoro, itapeleka nini Morogoro hakuna mtu wa Mwanza, Shinyanga, Tabora atakayeiona. Labda iwe ajenda ya 2025, reli hiyo itakapokuwa imekamilika kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma,” alisema Zitto.

Alisema katika uchaguzi huo CCM haiwezekani kuomba kura kwa gia ya mradi wa umeme wa Mto Rufiji wa Stigler’s Gorge kwa madai kuwa hautakuwa ukizalisha hata uniti moja ya umeme.

“Watakwenda kuuza matumaini. Watu watapiga kura kwa sababu ugali wao umepungua, sukari kutoka Sh1,800 kilo hadi Sh3,000.”

“Kwa ajenda ya uchaguzi, wapinzani tunayo ila tusipojenga hoja imara kama wapinzani, CCM itapita kama inatutazama maana hakuna mmoja anayeweza kushinda uchaguzi,” alisema Zitto.

Alipoulizwa kama aliyoyasema ndio ajenda ya upinzani kwa ujumla, alisema, “jambo hili ni kwa wapinzani wote si Zitto pekee, hicho ndicho tunachokiamini.”

Kuhusu kauli yake kuwa 2020 wapinzani wana turufu mbili kubwa za kuwaeleza wananchi wakati wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa alisema, “huo ni mtazamo wangu, lakini pia ni mtazamo wa ujumla wa wapinzani.”

Kuhusu hatima ya ubunge wake sambamba na wabunge wengine wa upinzani, alisema, “hatima ya wabunge ipo kwa wananchi, wananchi ndio wataamua kama wanafaa kuwawakilisha au wamefanya vibaya.

“Sina wasiwasi na maamuzi ya wananchi. Tumeweza kutimiza wajibu wetu kadri ya uwezo wetu na tumeweza kusukuma miradi ambayo inaweza kuisaidia Manispaa ya Kigoma Ujiji.

“Ambayo yametushinda kufanya tuna sababu zilizotokana na vikwazo vya uendeshaji wa nchi licha ya sisi kuwa na changamoto. Mazingira ninayoyaona nafasi ya wabunge wa upinzani 2020 ni kubwa.”

Alisema wapinzani wamekuwa watetezi wazuri kwa wavuvi na wakulima. “Naamini uchaguzi ukiwa huru na haki, si wabunge wa upinzani kuongezeka bungeni ila hata uwezekano wa CCM kubaki madarakani utakuwa mdogo.

“Nawauliza wananchi hali yao ni bora kwa sasa kuliko 2015 na wengi wanasema hali ya sasa imekuwa ngumu ila hakuna anayesema itakuwa bora sababu inajengwa reli ya kisasa, barabara za juu au uwanja wa ndege. Hakuna mwananchi anayeonyesha matumaini,” alisema Zitto.