VIDEO: Wabunge CCM, Chadema watoana jasho bungeni

Muktasari:

Unaweza kusema mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mwaka 2019/20 jana jioni Jumatano Aprili 10, 2019 jijini Dodoma ulitawaliwa na ‘vita’ ya maneno kati ya wabunge wa CCM na Chadema kutokana na wawakilishi hao wa wananchi kutumia mjadala huo kuikosoa na kuishauri Serikali, wengine kuitetea na kueleza ilichokifanya hadi sasa.

Dodoma. Wakati wabunge wa Chadema wakiikosoa Serikali na kuishauri njia nzuri ya kufanya kwa maendeleo ya Taifa, wenzao wa CCM waliwapinga na kutoa mifano ya utekelezaji wa mambo mbalimbali unaofanywa na Serikali.

Kwa kifupi unaweza kusema wabunge hao walichuana bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mwaka 2019/20 jana jioni Jumatano Aprili 10, 2019 jijini Dodoma.

Mara kadhaa mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alilazimika kuingilia kati na kuwatuliza wawakilishi hao wa wananchi ambao hawakusita kuomba taarifa kwa kiti na kutoa ufafanuzi kwa mzungumzaji kila walipoona hoja iliyotolewa haikuwa sawa.

Akizungumza katika mjadala huo mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema matokeo ya uamuzi unaofanywa na Serikali ni muhimu kuliko uamuzi husika, kutolea mfano jinsi sheria na mambo mbalimbali yanayopitishwa bungeni na maeneo mengine yanavyoibua hali ya sintofahamu nchini.

Amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imefanya uamuzi mkubwa katika mambo matatu, mengine madogo yasiyopungua 10 na kwamba mambo mengi yalifanyika bila kuzingatia matokeo yake yatakuaje.

“Serikali ilifanya uamuzi kuhusu kikokotoo, korosho, muswada wa habari, muswada wa takwimu, kutofanya kazi na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), muswada wa vyama vya siasa, Stiegler’s Gorge (mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji), reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege na kuhamia Dodoma,” amesema Mchungaji Msigwa na kuongeza:

“Moja ya sifa ya viongozi duniani ni pamoja na kufanya uamuzi sina tatizo na hilo, lakini tunapaswa kujua kama taifa matokeo ya uamuzi tunaofanya ni ya muhimu zaidi kuliko uamuzi tunaoufanya. Hatuishi kwa uamuzi tunaoufanya dakika moja, tunaishi kwa matokeo ya uamuzi tunaoufanya.

Amesema kabla ya kufanya uamuzi watu wenye busara na hekima lazima wajifunze kwa kufanya utafiti, kupitia taarifa za kihistoria na kutazama wengine wamefanya uamuzi gani katika mambo wanayokwenda kuyafanya.

Msigwa alitolea mfano mambo hayo na kubainisha kuwa baadhi sheria zililetwa bungeni na kupitishwa lakini zimekuwa mwiba kwa wananchi, akitolea mfano suala la korosho na kikokotoo.

Mbunge wa Serengeti (CCM), Marwa Chacha alipopata nafasi ya kuchangia mjadala huo alipingana na Mchungaji Msigwa.

“Kuna mbunge mmoja alizungumzia kuhusu uamuzi, eti anasema kununua ndege ni uamuzi mbaya, hivi aliyekuwa akiipiga Serikali kwa nini nchi haina ndege si ni Msigwa? Sasa ndege zimenunuliwa anaanza kupiga kelele hawa watu vinyonga,” amesema Chacha.

“Kuna mtu anapinga Stiegler’s Gorge lakini tunajua umeme jinsi unavyokatika kwa sasa, umeme rahisi ni wa maji, labda upinzani mfanye utafiti mtwambie umeme rahisi ni wa gesi, huo utafiti mmefanya lini Msigwa?”

Kuhusu kikokotoo Chacha amesema sheria hiyo ilipitishwa bungeni na Msigwa akiwapo lakini Rais aliona si nzuri akabadili uamuzi: “hili ni jambo zuri.”

Naye mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka aliyejikita zaidi  katika utawala bora amesema: “Kila mmoja analia maana mawaziri wote bajeti zao utekelezaji wake ni asilimia 70, tumefika ndani ya Bunge tunafanya siasa.”

Amesema utawala bora tafsiri yake ni maisha mazuri ya wananchi: “Unategemeaje maendeleo wakati wananchi wanabaguana na kikundi kimoja kinaonekana bora kuliko kingine. Taifa linatakiwa kuwa pamoja na kama halitakuwa pamoja tusitegemee maendeleo na wawekezaji.

“ Tunatakiwa kuwa pamoja na tutambue kuwa demokrasia ni jambo kubwa, demokrasia ni maendeleo na CCM mnachokifanya ni kwa ajili ya uchaguzi ujao si maendeleo, mnafanya kwa ajili ya siasa ya kesho na wananchi wanazidi kulia.”

Amesema wakulima, walimu na wafanyabiashara wanakumbana na changamoto na shida mbalimbali,  wamekaa kimya kwa sababu wakizungumza wanakamatwa na kuwekwa ndani huku wanasiasa nao wakibanwa.

Mbunge huyo amesema CCM wameanza kuchekana wenyewe kwa kuzungumzia mazuri mengi  yamefanyika katika Serikali ya Awamu ya Tano.

 “Hivi Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa ya Chadema? Hivi nyie Awamu ya Tano mngejenga chuo kikuu cha Dodoma tungelala na kunywa maji kweli?  Leo mnazomeana Awamu ya Nne na ya Tano. Wekeni mipango ya muda mrefu ya maendeleo na si kuzomeana” amesema Mwakajoka.

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Khamis Gulamali alimpa taarifa Mwakajoka, akimtaka ajikite zaidi kuzungumza matatizo ya jimbo lake kama maji na barabara na si kukosoa.

“Huyu bwana mdogo siwezi kupokea taarifa yake naona ana matatizo,” amesema Mwakajoka na kubainisha kuwa hata waziri wa Fedha amesema bungeni kuwa hakuna fedha na  hawezi kusifia chochote wakati hakuna kazi iliyofanyika.

Kauli hiyo ilimnyanyua Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashantu Kijaji, “Anaposema waziri wa fedha alisimama na kusema hakuna fedha lakini amesikia vituo vya afya zaidi ya 352 vimejengwa ndani ya mwaka mmoja. Tayari  tumeshatoa zaidi ya Sh2trilioni kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa.”

“Sh1.5bilioni zimetolewa kwa hospitali za halmashauri 67, fedha ipo na Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo aseme mambo ya ukweli ambayo wananchi wanayaona kwa macho yao, Serikali inatekeleza miradi ya maendeleo katika majimbo yote, likiwemo  jimbo lake.”

Akijibu taarifa hiyo Mwakajoka amesema, “Tukiangalia  takwimu za mwaka jana za vifo vya wanawake na watoto kati ya vizazi 100,000, watu wanaopoteza maisha ni vizazi 65,000, karibu 44,000 ndio wanakuwa wazima, eti anasema unajenga vituo, unajengaje vituo (vya afya) dawa  na vifaa hakuna una maana gani?”

Mwakajoka alirejea tena hoja yake ya utawala bora, “niwambie CCM wananchi hawajakaa kimya kwa sababu wameridhika na utawala huu, wanajua mnategemea katika uchagazi ujao mtapeleka polisi ila wamesema hawatagombana na polisi watakwenda kujuana na ndugu zao watakaosababisha wapigwe.”

“Mnataka kuleta machafuko katika nchi hii kwa sababu ya uroho wa madaraka haiwezekani mmekubali demokrasia leo mnataka mbaki peke yenu wakati wananchi hawakubaliani na nyinyi wanataka upinzani ndani ya nchi.”

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia alisimama na kuomba taarifa akimpinga Mwakajoka, “Namuheshimu  Mwakajoka, si kweli kwamba wananchi hawaipendi CCM ni kwamba wananchi huko tulikotoka wameridhika na wanakipenda CCM na 2020 hali itakuwa mbaya sana kipande cha kule (upinzani).”

Wakati Zungu akimhoji  Mwakajoka kama amekubali taarifa hiyo, mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko nae alisimama na kuomba taarifa.

“Anayoyasema Mwakajoka ni kweli bila polisi CCM haitafika madarakani  na uthibitisho upo katika kata ya Tua kule Tarime (katika uchaguzi wa diwani)  tuliwashinda  CCM kwa zaidi ya kura 76 lakini walipiga mabomu wakachukua wakajitangaza ,” amesema Matiko.

Mwakajoka alikubali taarifa hiyo na kusisitiza, “Ninaipokea hata kwetu Momba mkurugenzi alikuwa na polisi zaidi ya 100 katika chumba na alinyang’anya matokeo akaondoka nayo, kama Mtulia anasema CCM inapendwa na wananchi wekeni mpira chini.”

Naye mbunge wa Monduli (CCM),   -amesema, “Tusikatishwe tamaa na maneno ya watu waliokata tamaa wenyewe, ukimkuta binadamu asiyeshukuru hata jambo moja ujue amekata tamaa mwenyewe au hajui anachotakiwa kushukuru au kupinga. Ni ngumu sana kuamini wapinzani wote katika Bunge hili wana akili sawa.”

Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga aliomba taarifa akipingana kauli ya Kalanga, kwa madai kuwa mbunge huyo wa Monduli ndio aliyekata tamaa kwa sababu alikimbia Chadema na kujiunga  CCM, na huko ni sawa na kujisalimisha.

 “Hiyo sio taarifa,” amesema Zungu na kumtaka Kalanga kuendelea kuchangia mjadala huo.