Wabunge wachachamaa mazingira ya biashara nchini

Mbunge wa Busega (CCM), Raphael Chegeni akihoji kufugwa kwa biashara nyingi nchini wakati akichangia mjadala bungeni wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Hoja za biashara kufungwa, kutoanza kwa miradi ya kufua chuma ya Liganga na Mchuchuma na utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa mambo yaliyotikisa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2019/20.

Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo juzi jioni, wabunge waliitaka Serikali kuangalia upya maeneo mbalimbali ili kuboresha uchumi nchini.

Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema kuanzisha biashara Tanzania ni mzigo akisema utatozwa kodi ambazo ni mtaji.

Alisema Watanzania wamezoea kuitana majina ya fisadi, mwizi na kuwataka kujiuliza kama ameweza kuiba na kuwekeza nchini wizi wake uko wapi? “Tunavunjana moyo Watanzania,” alisema Chegeni.

Alisema hata wageni wanaonekana kuwa ni tatizo na kuhoji, “unawezaje kujenga uchumi wa nchi moja peke yako?

“Naomba nimnukuu Naibu Waziri wa Fedha (Dk Ashatu Kijaji) alisema, biashara nyingi zinafungwa lakini nyingi zinafunguliwa. Sio kweli biashara nyingi zinafungwa… Tunapaswa kama nchi tujitathmini upya why (kwa nini) bila kufanya vile unapataje hiyo kodi?” alihoji.

Baadaye jana, Dk Kijaji akijibu hoja hiyo alisema si kweli kwamba biashara nyingi zimefungwa na kubainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Aprili, biashara zilizofungwa zilikuwa ni 16,252 na zilizofunguliwa ni 147,818.

Lakini, Dk Chegeni pia alimtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kuitumia nafasi aliyopewa na Rais John Magufuli kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi akisema, “leo hii ukienda by statics makusanyo ya kodi ya TRA yanazidi kushuka. Mkatae msikatae yanashuka. Yanashuka kwa sababu lazima tuchochee tupate biashara nyingi.

“Msaidieni kufanya kazi hizi, haiwezekani Rais anazunguka anapiga kelele mpaka anasema hamnielewi, kama hamumuelewe basi achieni ngazi. Tunataka Tanzania ambayo inasonga mbele,” alisema.

Kuhusu makusanyo, Dk Kijaji alisema kutokana na kuongezeka kwa biashara, mapato kwa kila mwezi yamekuwa yakiongozeka na kwamba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba 5, 2015 hawajawahi kukusanya mapato ya chini ya Sh1 trilioni kwa mwezi.

Dk Chegeni alisema muonekano wa kwanza wa mtu anapokuja nchini ni watu wa uwanja wa ndege, lakini akasema huwa “wamenuna kama wamekula pilipili.”

Kauli hiyo ilijibiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kupitia taarifa, akisema kazi ya kuwafanya watumishi wa uwanja wa ndege kuwa na tabasamu inafanyika.Alisema wameanza na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kuajiri warembo wenye tabasamu.

Lakini akijibu taarifa hiyo, Dk Chegeni alisema waziri hakumuelewa alichomaanisha akisema ni utamaduni wa kupokea wageni.

Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia aliitaka Serikali kupunguza muda wa majadiliano inapopata wawekezaji. “NDC (Shirika la Maendeleo la Taifa) kila ukiuliza nini kinaendelea huko wanasema majadiliano yanaendea.”

Alisema kupitishwa kwa sheria mpya za rasilimali za Liganga na Mchuchuma, kumefanya majadiliano ya miradi hiyo kuanza upya.

Ghasia alisema kama miradi hiyo ingekuwa imeanza kwa wakati, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ungejengwa kwa kutumia chuma kinachozalishwa na miradi hiyo badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Hawa Mwaifonga alisema TRA imekuwa mwiba mchungu kwa wafanyabiashara na si rafiki tena wa mlipakodi.

“TRA wamekuwa wababe, hawataki kumsikiliza mtu, wamesababisha biashara kufungwa, viwanda kufungwa. Leo nilikuwa namsikia mtu mmoja anasema biashara zaidi ya milioni moja zimefungwa, huo ndiyo ukweli,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wabunge akiwamo wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Lulida aliyetaka TRA ifumuliwe.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Kiteto Koshuma alisema anaunga mkono mfumo wa kukusanya kodi kwa njia ya kieletroniki lakini unagharama kubwa. Alisema kodi ya juisi aina ya kijoti ni Sh3, lakini gharama ya kukusanya kodi hiyo ni Sh9 kwa kila kijoti na kuhoji kama inaingia akilini, “ninaomba kuiuliza Serikali ilitumia mfumo gani kumpata mzabuni aliyeweka hii teknolojia?

Mbunge wa Mfenesini (CCM), Kanali mstaafu Masoud Ali Khamis alisema kuna viwanda vinavyoweza kuzalisha bidhaa zinazotosheleza nchini lakini bado bidhaa hizo zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

“Tufike mahala tuamue kama tunataka kujenga viwanda tuwe tayari kuwalinda wale wenye uwezo wa kuzalisha,” alisema.

Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalaly Kafumu alitaka kila sekta kuangalia sheria zake zilizofukuza wawekezaji nchini.

“Sheria ni nzuri zinalinda rasilimali zetu, lakini kuna vipengele akisoma tu mwekezaji anabwaga manyanga anaondoka. Naomba sana waziri wa sheria na wa madini hebu angalieni kuna vipengele vichache ukivibadilisha kidogo unahamasisha uwekezaji,” alisema.

Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael alisema ukiangalia maneno ya viongozi wakuu ni kama Serikali imeamua kujenga viwanda na kufanya biashara yenyewe.

“Kweli unaonyesha kuwa Serikali inataka kuonyesha wananchi kuwa wenyewe ndiyo wanataka kufanya biashara, ifanye kazi ya kujenga viwanda. Leo inaonyesha kuwa mnakatisha tamaa sekta binafsi.”