Wadau wajadili kumpumzisha Kairuki kwenye uwekezaji

Muktasari:

  • Baada ya Rais Magufuli kusema kuwa amempeleka Waziri Angela Kairuki ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) ili akapumzike kwa kuwa hakuwa mkali akiwa Wizara ya Madini, baadhi ya wadau wa uchumi wamedai kwamba wizara aliyohamishiwa Kairuki ina majukumu mazito.

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akisema amempeleka Waziri Angella Kairuki Ofisi ya Waziri Mkuu kushughulikia Uwekezaji ili akapumzike kwa kuwa hakuwa mkali alipokuwa Madini, baadhi ya wadau wamesema huko alikopelekwa ndiko kwenye majukumu mazito zaidi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akihutubia mkutano mkuu wa kisekta wa Wizara ya Madini, jijini Dar es Salaam, huku akimtaka Waziri wa Madini, Doto Biteko kuwa mkali.

“Na kwenye wizara hii nakwambia Waziri Biteko uwe mkali, aliyekuwa waziri mwenzako hakuwa mkali. Naficha nini? Ndiyo maana nikamwona ngoja akapumzike ofisi ya waziri mkuu pale. Nawaeleza ukweli, that’s me,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati tayari ameshawatema mawaziri tisa katika miaka mitatu tangu aingie madarakani, huku akisema hivi karibuni kuwa hatajali kubadilisha mawaziri hata kama ni kila siku.

Mawaziri walioenguliwa kwa makosa mbalimbali tangu Magufuli aingie madarakani Novemba 5 mwaka 2015 ni pamoja na Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani), Nape Nnauye (Habari), Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani), Dk Charles Tizeba (Kilimo) na Charles Mwijage (Viwanda).

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge na Profesa Jumanne Maghembe (Maji).

Manaibu Waziri walioachwa ni pamoja na Annastazia Wambura (Habari), Ramo Makani (Maliasili na Utalii) na Dk Suzan Kolimba (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda.)

Akishikilia wizara mbalimbali zikiwamo za Ofisi ya Rais (Utumishi) na baadaye Madini kabla ya kupelekwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Kairuki, ametajwa kutokuwa mkali.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa uchumi wamesema wizara hiyo mpya kwa Kairuki itakuwa na majukumu mazito.

Mkurugenzi wa Taasisi ya sekta Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema kwa muda mrefu kitengo cha uwekezaji kilikuwa kimewekwa mahali pasipo pake katika Wizara ya Viwanda na Biashara na Uwekezaji.

“Kwanza ujue kwa nini Rais ameunda ile wizara, ni jambo linalofanyika hata nje ya nchi, kwamba inakuwa na mamlaka zaidi, tofauti na ilikokuwa kule Wizara ya Viwanda na Biashara,” alisema Simbeye.

‘Tunategemea tutakuwa na waziri ambaye kila siku atakuwa na jukumu moja la uwekezaji na atakuwa anapeleka taarifa za uwekezaji kwenye Baraza la Mawaziri,” aliongeza.

Alisema Kairuki amewekwa katika wizara hiyo wakati Kituo cha Uwekezaji (TIC) kikiwa na changamoto kubwa, za ukosefu wa bajeti ya kutosha, wafanyakazi na mamlaka ya kitaasisi.

Maoni kama hayo pia yametolewa na Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi akisema Kairuki anatakiwa kuhakikisha kunakuwa na sera, sheria na mazingira bora ya uwekezaji.

“Tanzania tumefanikiwa sana kualika wawekezaji, lakini wanapokuja hawakai kwa sababu ya kukosekana kwa sera, sheria na mazingira bora na akiondoka mmoja anapeleka ujumbe kwa wenzake,” alisema Profesa Ngowi.

Alitaja mambo muhimu katika uwekezaji kuwa pamoja na kodi, miundombinu na nishati akisema waziri huyo anapaswa kuyaboresha ili wawekezaji waje na wakae.

Kwa upande mwingine akizungumzia kauli ya Rais kwamba amempeleka waziri huyo kupumzika, Mkurugenzi mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hilo si suala la ajabu.

“Utakuta huyu amelewa anafukuzwa, wengine wanaachwa, wanaotakiwa kuondolewa wanaachwa, wanaotakiwa kuonywa tu wanafukuzwa,” aliongeza.

Mbunge wa Tarime Vijijini ambaye pia ni Waziri kivuli wa Madini, John Heche alisema ameshangazwa na kauli ya Rais kuwa amempeleka Waziri Kairuki kumpumzika.

“Wizara ambayo tunakaribisha wawekezaji, walete ajira, mitaji na miradi mbalimbali ndiyo umpeleke waziri akapumzike? Rais anasema hatavumilia mtu, lakini anapeleka mtu kupumzika?” alihoji Heche.

Akizungumzia sekta ya madini, Heche alisema kinachotakiwa ni kushirikisha wadau na kufuata sheria ili kuhakikisha madini yanwanufaisha wananchi.