‘Wajanja wamegawana pikipiki alizotoa Diamond’

Saturday May 25 2019

pikipiki , Diamond,WCB,Babu ,Tale ,mwananchi, Harmonize ,

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Huenda umejiuliza pikipiki 20 ambazo mwanamuziki Diamond Platnumz, alizitoa mwishoni mwa mwaka jana zimezalisha nyingine ngapi mpaka sasa kama ilivyokuwa matarajio yako. Jibu ni sifuri.

Mwaka jana, mwanamuziki Diamond mbali na kutoa bima za afya kwa wakazi 1,000 wa eneo la Tandale, jijini Dar es Salaam, alitoa pikipiki 20 kwa vijana katika mpango wa kuwawezesha.

Katika hafla hiyo pia alimkabidhi mwanamke mlemavu zawadi ya bajaj ambaye alimuona kupitia kipindi cha televisheni cha Wasafi akieleza anavyopata wakati mgumu kuendesha maisha.

Diamond alitaka pikipiki hizi zizalishe nyingine ili ziweze kuajiri vijana wengine wengi zaidi kwa kuweka utaratibu wa kupeleka hesabu kila wiki na fedha hiyo inunue pikipiki nyingine zaidi.

Matarajio yake yamekuwa kinyume kwani hata uongozi wa WCB haufahamu pikipiki hizo zipo wapi.

Mmoja wa mameneja wa mwanamuziki huyo, Hamis Tale maarufu Babu Tale amesema kumetokea sintofahamu ya pikipiki hizo na mpaka sasa wameamua kuacha kuzifuatilia.

Advertisement

“Kwa kifupi ninaweza kusema watu wasiokuwa na nia njema na maendeleo wameamua kugawana pikipiki hizo na tumejaribu kufuatilia tukaona tutajenga uhasama bure wakati lengo la Diamond lilikuwa kutoa msaada,” amesema Babu Tale.

Ameongeza kuwa lengo la Diamond lilikuwa kuwainua vijana wenzake na bado nia hiyo anayo hivyo atakuwa makini zaidi wakati mwingine.

“Unajua wewe unapofikiria kupiga hatua, wengine wanaangalia namna gani watakuangusha. Tulitarajia pikipiki zile ziwe zimeajiri vijana wengi mpaka sasa lakini watu wasio na nia njema wameamua kufanya yao, hatukati tamaa tutatafuta namna nyingine ya kufanya siku nyingine,” amefafanua.

Kuhusu bifu la Harmonize, Diamond

Hivi karibuni mwanamuziki Harmonize kupitia mtandao wa Instagram alimtupia kijembe Diamond kufuatia mashairi yake katika wimbo Inama akisema mpenzi wake Sarah alitoka na baunsa wake, Mwarabu Fighter alisema hakuna kitu kama hicho.

Pia, zimekuwapo tetesi kwamba mwanamuziki huyo wa kwanza kusimamiwa na Diamond amekuwa katika msuguano na bosi wake.

“Nasra (mwandishi) unaamini Harmonize aliusikia wimbo baada ya kutoka? Unajua kabisa WCB hakuna msanii anaweza kutoa wimbo bila kusikilizwa na wenzake kwa hiyo hakuna kitu kama hicho,” amesema.

Kuhusu Harmonize kufuturisha nje ya WCB alisema mwanamuziki huyo ni sehemu ya mradi wa kampuni hivyo chochote anachofanya kinapata baraka kwa kuwa mwisho wa siku kinapeleka faida kwenye mfuko wao.

Amesema kwa mwaka huu WCB itafuturisha katika mji wa Kahama na Harmonize amefuturisha jijini Dar es Salaam jana akiwa na baraka za kampuni.

“Popote unapomuona Harmonize anafanya kazi jua kinainufaisha WCB, ni kijana wetu anayejituma sana hivyo hayo maneno unayosikia huko ni ya watu tu wanaotafuta habari mpya za kuzungumza kila siku,” amesema.

Advertisement