Wanafunzi waeleza wanavyorubuniwa, kupewa ujauzito

Muktasari:

  • Wanafunzi wa kike wameeleza jinsi wanavyorubuniwa ikiwamo kununuliwa chips na wanaume ambao huwavizia wakati wakitoka shule huku wakiwapa ahadi kemkem ikiwamo hata kujengewa nyumba.

Dar es Salaam. Wanafunzi wa kike wameelezea namna wanaume wakware wanavyowarubuni na kusababisha baadhi yao kupata ujauzito na kulazimika kukatisha masomo.

Wanafunzi hao walifunguka wakati wa kampeni ya kupambana na tatizo la ndoa na mimba za utotoni inayoendeshwa na Shirika linalojishughulisha na masuala ya kisaikolojia kwa watoto (REPSSI) katika vijiji na mitaa iliyo pembezoni kwa barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Simulizi za wanafunzi hao katika maeneo tofauti ziliwafanya wapigwe butwaa kutokana na kutotaja sababu za mimba.

Lakini mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Bungu B, Kibiti mkoani Pwani aliweka bayana mbinu hizo baada ya kuulizwa sababu za tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

“Wengi hujikuta wakiangukia kwenye mitego kutokana na ahadi kemkem,” alisema huku akishangiliwa.

“Ngoja mie niseme ukweli. Utakuta baba anakukaribisha chipsi wakati huo umetoka shule una njaa na nyumbani ni mbali. Ukila tu anaanza kukuahidi kuwa ukiwa mkubwa atakujengea nyumba na kama utakubali anachotaka mara atakuwa anakupa hela za nauli shuleni.

“Mimi ni mtoto ila kuna mtu mkubwa aliwahi kuniambia ujinga nikamsemea kwa mama akasema nisikubali tena kusikiliza hao watu waongo, wabaya. Wakiniharibu watakimbia.”

Alisema wasichana wanatakiwa kutimiziwa mahitaji yote muhimu ili isiwe rahisi kurubuniwa.

“Ukipata mimba unafukuzwa shuleni na nyumbani wazazi hawakuelewi lakini njiani vishawishi vinazidi uwezo wa mtoto kuhimili,” alisema.

Ofisa maendeleo ya jamii wa kata ya Bungu, Johnmary Richard alisema ni kweli vishawishi vya baadhi ya wanaume wakware kwa watoto wa kike vinawafanya baadhi yao kushindwa kuhimili.

Alisema kinachotakiwa kufanywa ni watoto wa kike kujengewa ujasiri wa kuwashtaki wanaume wanapojaribu kuwashawishi ili sheria ichukue mkondo wake.

Mkurugenzi wa REPSSI, Edwick Mapalala aliwashauri wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili wanapokutana na mambo magumu katika makuzi yao, iwe rahisi kuwaeleza bila woga.

Aliwataka kuwa makini katika kuhakikisha wanawatimizia mahitaji yote muhimu ikiwamo chakula shule ili isiwe rahisi kutegwa.

Mmoja wa wazazi katika kata hiyo, Aman Pazzi alisema kama mtoto anatembea umbali mrefu wakati ana njaa, ipo hatari kubwa ya kurubuniwa na kuingia kwenye vishawishi.

“Kuna wazazi wakiona mtoto amekua hata kwa miaka 14 anaona bora amuozeshe asilete aibu nyumbani, lakini akimlea kimaadili na kutimiziwa mahitaji hofu itaondoka,” alisema.

Mwanafunzi mwingine wa Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nyamisati, alisema wanaume huwasubiri wanapokuwa wakitoka shule.

“Hata mimi nakaa chumba cha kupanga kuna mitego mingi sana ya wanaume. Wengine ni wakubwa kabisa,” alisema.

“Binafsi kuna wakati chakula kinaisha wazazi hawajanitumia. Inabidi nikope dukani na wakati mwingine nakaa na njaa natamani kutimiza ndoto zangu kama mama Samia Suluhu ( Makamu wa Rais),” alisema.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Sofia Mnyasi alisema mara nyingi wanapokutana na vishawishi hivyo, baadhi yao hushindwa kuhimili.

“Nina ndoto yangu madhubuti ndio maana naweza kusema, lakini wenzetu wakibanwa sana hushindwa,” alisema Sofia.

Kwa upande wake, Magreth Justine, mwanafunzi wa Sekondari ya Wama, alisema ni wakati wa wazazi na Serikali kuweka mazingira mazuri ya elimu ili kuondokana na vishawishi hivyo.

Ofisa maendeleo ya jamii wa Kata ya Salale, Sikudhani Nyambagi alisema kuna mazingira magumu yanayosababisha vishawishi kwa wanafunzi wa kike.

“Wamepanga vyumba na hali mbaya wakikutana na vishawishi wakati wana mahitaji ya msingi kama kodi, chakula na hata taulo za kike,” alisema.