Wanaume waaminifu tupo, ila tatizo letu hatuna fedha

Mke na mume waligombana, nyumba ikageuka kuwa uwanja wa vita ya tatu ya dunia. Kila mmoja anamtupia mwenzie nyuklia za maneno lakini mwanaume akaishiwa nguvu mapema sana – akanyamaza.

Mwanamke akaendelea. “Mwanaume gani wewe, huna hata haya. Najuta kuolewa na wewe, mara 100 ningeolewa na shetani, kuliko mtu wa ovyo namna hii.”

Mwanaume akajibu. “Ungeolewa na shetani, lakini hairuhusiwi mtu na kaka yake kuoana.” Nina uhakika unajua kilichoendelea.

Kwa mujibu wa baadhi ya wanawake; wanaume wote ni mbuzi (kimsingi, sio mbuzi, kuna jina la mnyama mwingine wanalotuita ambalo nikiliandika hapa gazetini, hii inaweza kuwa Makala yangu ya mwisho kuchapishwa.

Tafsiri yake ni kwamba? Haturidhiki hata tupewe nini, hatuna aibu na tumekosa uaminifu kabisa. Kwamba mwanaume mpatie kila kitu anachostahili kupewa, mpe na vya ziada lakini linapokuja suala la kuwa mwaminifu na ndoa au uhusiano lazima atavuka mipaka tu, atatoka nje.

Tusikatae, yawezekana ikawa kweli, kwamba kuna wanaume si waaminifu, lakini mashaka yanakuja pale unapogundua mwanamke anayesema wanaume ‘wote’ ni mbuzi, hajawahi kuwa na uhusiano na hata nusu ya wanaume wa mtaa anaoishi – suala la wote linatokea wapi?

Wanawake wanakosea kuelewa, tatizo hapa halipo kwa wanaume, lipo kwenye asili ya binadamu. Roho zetu ziliumbwa na kitu kupenda, kupenda vitu vizuri. Kuna wakati binadamu anapopenda kitu kizuri anaweza kufanya chochote ilimradi apate, roho yake itulie.

Tafsiri yake ni kwamba, hapa tatizo linaweza lisianzie kwa mwanaume, likaanzia kwa wanawake wengine huko nje. Kwa sababu labda mwanaume ana kitu kizuri wanachopenda wanawake mathalani pesa. Unaweza kukuta wanawake wanaanza kutengeneza mazingira ya kukipata bila kujali hali ya uhusiano wa mwanaume, kwamba ameoa, ana mchumba au vipi. Hiyo kwake haimhusu, ishu ni ana pesa, anazitaka.

Kwa hiyo mwanaume anapokutana na majaribu mengi ya aina hii, kama imani yake ni ndogo, unakuta ni rahisi sana kufanya vitu vya ajabu.

Hii inaweza kuwa sawa na kwa wanawake; baadhi ya wanaume tunasema wanawake si waaminifu, lakini kimsingi inawezekana kuna wanawake waaminifu ni wengi sana, tatizo hawana mambo tunayoyapenda – mathalani mawowowo.

Kwa hiyo, wenye nayo, wanapitia changamoto za kama mwanaume mwenye hela, kwamba kila mtu huko nje anawasumbua kutaka kupata walichonacho, kwa hiyo kama mwanamke moyo wake haujamjaza Mungu kisawasawa unakuta suala la kuwa muaminifu kwake linakuwa mtihani mgumu sana – anakengeuka.

Kumbe si wanaume wote wabaya, waaminifu tupo ila hamtuwazi kwa sababu tu hatuna fedha. Kama ambavyo kuna wanawake waaminifu ila hawaonekani kwa sababu hawana mawowowo.