Washtakiwa saba mauaji ofisa polisi waachiwa

Thursday May 16 2019

 

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imewaachia huru watu saba waliokuwa wanakabiliwa na shtaka la kumuua kwa makusudi sajini wa polisi, Abdallah Chande, kwa kumkata mapanga mwaka 2017.

Baada ya Jaji Patricia Fikirini kutoa uamuzi huo, ndugu wa marehemu waliokuwapo mahakamani hapo na mke walishindwa kujizuia na kububujikwa machozi.

Walioachiwa huru ni Goodluck Shuma maarufu Manyama, Gasper Mushi au maarufu Paruu, Edward Mushi au Baba Obama na Philip Temba ambaye anajulikana pia kama Ndorambalo au Ndorobo.

Wengine kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa kortini na mawakili wa Serikali; Isack Mangunu na Ignas Mwinuka, ni Petro Mushi, Twalib Moshi au Kibunduki na Mussa Shaaban au Abasii.

Siku ya mauaji Machi 17, 2017 saa 12:30 jioni, inaelezwa kuwa marehemu ambaye alikuwa amevalia kiraia, alikwenda nyumba moja ya wapika gongo na kuomba apewe Sh5,000.

Kulingana na ushahidi huo, washtakiwa hawakupendezwa na kitendo cha polisi huyo kuomba fedha hizo ambako wanadaiwa kumshambulia kwa mapanga hadi kufariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa KCMC.

Uchambuzi wa jaji

Katika hukumu yake, Jaji Fikirini alisema ushahidi wa mashahidi sita wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa bila kuacha shaka, hivyo anawachia huru.

Akichambua ushahidi huo, alisema baadhi ya ushahidi ulikuwa wa kujichanganya na kukinzana hasa katika kueleza nani alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio na nini kilitokea.

Jaji Fikirini alisema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka lakini umeshindwa kufanya hivyo na anawaachia washtakiwa wote waliotetewa na mawakili, David Shillatu na Charles Mwanganyi.

Katika tukio lingine, Jaji Fikirini amemwachia Ramadhan Kassim aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kusafirisha kilo 73 za mirungi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka.

Jaji huyo alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuita mashahidi wawili muhimu, koplo Ramadhan na Aisha Athman, ambao ndiyo wangeweza kumtambua mshtakiwa.

Advertisement