Watanzania 9 wafariki dunia kwa kupigwa risasi

Dar es Salaam. Watu 11 wakiwemo Watanzania tisa na raia wawili wa Msumbiji wamefariki dunia baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Mtole kilichopo upande wa nchi hiyo jirani.

Tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita usiku katika kijiji hicho kilichopakana na Kijiji cha Kiamba upande wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa na televisheni ya UTV Azam jana jioni, wakazi hao walikuwa wakifanya shughuli zao za kilimo katika kijiji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Akizungumza na UTV, mtendaji wa Kijiji wa Kiamba, Fadhili Makosa alisema “kwa sasa tunaendelea na taratibu za mazishi na tulikuwa na ndugu zao ambao wametambua maiti. Kila mwili uliotambuliwa umechukuliwa na ndugu husika.”

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema mauaji hayo yamefanyika Msumbiji ambako Watanzania walikwenda kujitafutia riziki ikiwemo kufanya kilimo cha mpunga katika kambi ambazo kila wakati huwa wanakwenda kufanya shughuli hizo.

“Walivamiwa na kupigwa risasi na wahalifu hao, nimewasiliana na IGP wa Msumbiji tutakutana kesho ili kuangalia eneo ambalo tukio limetokea.

“Hawa waliopoteza maisha taarifa nilizonazo walishakatazwa kufanya shughuli za kilimo katika kijiji hicho, lakini kwa sababu wamezoea hawakuweza kukubaliana na jambo hilo,” alisema Sirro.

Sirro aliwahakikisha Watanzania kuwa waliohusika na mauaji hayo watasakwa na kukamatwa kwa ushirikiano na Msumbiji huku akiwasihi wakazi wa Mtwara kama wana mpango kwenda Msumbiji kwa sasa wapunguze kidogo kwani hali si shwari.

“Wanaofanya haya mauaji haya wanazungumza Kiswahili kizuri sana na baadhi walikimbia Tanzania na kwenda huko. Lakini huwa nasema lugha moja ukiua Mtanzania ujue haupo salama popote ulipo, utakufa uliko au kurudishwa Tanzania uone dunia ilivyo,” alisema Sirro.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Dk Mathias Kisambo alisema juzi saa tano usiku walipokea majeruhi wanane walikokuwa na majeraha mbalimbali yaliyosababishwa na kushambuliwa na risasi hasa sehemu za mikono na miguu.

“Wengi waliumia miguuni na tuliwapeleka idara ya dharura kwa ajili ya matibabu ya awali kisha kupelekwa wodini. Lakini watatu walipelekwa chumba cha upasuaji, kwa ujumla hali zao zinaendelea vyema,” alisema Dk Mathias.