Watanzania tisa akiwemo Shikuba wahukumiwa kifungo Marekani

Muktasari:

Khatib Haji Hassan (49) maarufu Shikuba ni miongoni mwa Watanzania tisa waliohukumiwa kifungo nchini Marekani kwa kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin

Houston. Khatib Haji Hassan (49) maarufu Shikuba ni miongoni mwa Watanzania tisa waliohukumiwa kifungo nchini Marekani kwa kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin.

Tangazo lililotolewa na mwanasheria wa Marekani,  Ryan Patrick mbali na kuwataja Watanzania hao tisa, pia limewataja raia wawili wa Pakistan na Iran,  Salim Omar Balouch na Abdul Basit Jahangir.

Shikuba alipelekwa Marekani mwaka 2017 akitokea Tanzania kwa ajili ya kushtakiwa kwa makosa hayo.

Watanzania wengine ni Ernest Michael Mbwile (35), Abdulahtif Juma Maalim (43), Ibrahim Omary Madega (52), Tiko Emanuel Adam (41), Iddy Saleme Mfullu ( 46), Mohammed Said Mohammed (48) na Daud Michael Vedasto (58).

Taarifa iliyotolewa Jumatano Agosti 7, 2019 na Jaji Sim Lake wa Marekani ilikamilisha siku mbili za usikilizwaji wa kesi hiyo na kuwapeleka jela washtakiwa hao.

Katika hukumu hiyo, Jahangir amehukumiwa miezi 151 jela sawa na miaka 12 , huku Mfullu na Mohammed wakihukumiwa miezi 50 sawa na miaka minne jela.

Shikuba amehukumiwa miezi 99 jela sawa na miaka minane, Mwinyi, Mbwile, Maalim, Madega, Adam na Vedasto wamehukumiwa vifungo  tofauti vya miezi 52, 46, 87, 37 na 46.

Mahakama hiyo pia imemhukumu Balouch kifungo cha miezi 135 sawa na miaka 11 jela.

Kwa kuwa siyo raia wa Marekani, wafungwa hao watarejeshwa kwenye nchi zao baada ya kutumikia adhabu zao.

Kesi hiyo ilianza kwa kumkamata mmoja wao katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Houston’s Bush Intercontinental  Juni 3,  mwaka 2012.

Mshitakiwa huyo alikuwa amemeza kilo 1.5 za Heroin zilizofungwa katika pakiti 100.