Wazalishaji sukari wampinga waziri kuhusu vibali

Thursday February 14 2019

 

By Ephrahim Bahemu na Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Dar/Moshi. Wazalishaji wa sukari wa ndani wamesema si kweli kwamba viwanda vyao vimebweteka kwa kuwa wanaruhusiwa kuagiza sukari nje ya nchi, bali uzalishaji umeongezeka na bado wana nia ya kuongeza zaidi.

Akizungumza na wadau wa sekta binafsi na wa kilimo juzi, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema Serikali imeamua kusitisha vibali hivyo na badala yake itatumia kampuni nyingine, lengo likiwa ni kuwataka wazalishaji wa ndani kuongeza nguvu ya kuzalisha.

Alisema tangu kampuni hizo ziruhusiwe kuingiza sukari, zimeshindwa kuendeleza viwanda vyake ikiwamo hata kulima miwa ya kutosha kwa ajili ya malighafi na badala yake nguvu kubwa imeelekezwa katika kuagiza.

“Kama kuna wazalishaji walikuwa na mpango wa kuomba vibali wasahau kwa kuwa zoezi hilo limeshafungwa, sasa waendelee na uzalishaji pekee mpaka hapo utaratibu mwingine utakapowekwa,” alisema.

Alisema sukari iliyopo ina uwezo wa kuhudumia walaji nchini mpaka Mei na kuanzia Juni, Serikali itaagiza tani 25,000 hadi 28,000 ili kusitokee uhaba.

Kwa uamuzi huo, kiwanda cha Sukari cha TPC Limited cha Moshi, kushtushwa kikieleza kuwa hakuna mzalishaji wa ndani anayependa kuagiza sukari kwa kuwa uzalishaji wa ndani unalipa zaidi.

Ofisa mtendaji wa TPC anayeshughulikia utawala, Jaffary Ally alisema jana kuwa hatua ya Waziri Hasunga kutengua maelekezo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa mwaka 2017, kimewaacha vinywa wazi.

Ally alisema Waziri amefanya uamuzi huo bila kushauriana na wazalishaji wa sukari nchini ambao Rais Magufuli aliwapa dhamana ya kuagiza sukari nje na huku wakiendelea na juhudi za kuimarisha uzalishaji wa ndani.

“Sasa waziri kupindua maagizo ya Rais sisi imetuacha vinywa wazi! Huenda ni maagizo ya Rais mwenyewe! Lakini si kweli kwamba walipopewa kibali cha kuagiza sukari, wazalishaji wa ndani walibweteka na kuzorotesha uzalishaji siyo kweli kabisa,” alisisitiza.

Alisema takwimu zinaonyesha uzalishaji uliongezeka kwa zaidi ya tani 40,000 ikilinganishwa na mwaka wa nyuma kabla ya kupewa jukumu la kuagiza sukari na Rais.

“Kama maagizo ni kuondoa jukumu hili kwetu hatuwezi kuwa na kinyongo! Ila waziri ahakikishe Watanzania wanaletewa sukari safi inayofaa kwa matumizi ya binadamu na iwe kwa kiwango.”

Mkurugenzi wa mauzo na masoko wa TPC, Allen Maro alisema kama kweli serikali inataka wazalishaji wa ndani watosheleze mahitaji ya ndani, haina budi kuwatengea ardhi kwa ajili ya ulimaji wa miwa ya kutosha.

Mwenyekiti wa bodi ya kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Balozi Ami Mpungwe alisema Serikali inapaswa kuwa makini katika suala la muda wa kuagiza bidhaa hiyo, kiasi na kodi inayotozwa ili kulinda viwanda vya ndani, lakini pia soko la ushindani.

“Kwetu sisi wazalishaji kampuni yoyote itakayopewa tenda ya kuagiza hatuna tatizo nayo kwa sababu uagizaji sisi sio biashara yetu ya msingi. Sisi ni wazalishaji kikubwa ni ushindani wa haki sokoni,” alisema Balozi Mpungwe.

Alisema Kilombero sasa inasubiri ruhusa ya Serikali ili iongeze uzalishaji wake mara mbili kutoka tani 125,000 kwa mwaka hadi tani 250,000.

Advertisement