Waziri atengua kauli yake vibali vya sukari

Muktasari:

Baada ya kutangaza kutotoa vibali kwa wazalishaji wa sukari kuagiza nje ili wajikite katika uzalishaji, waziri wa kilimo, Japhet Hasunga amesema baada ya tathmini, wameamua kampuni hizo zipewe vibali ili kukidhi mahitaji ya tani 215,000 kwa matumizi ya kawaida kwa mwaka.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga jana alitengua kauli yake kuhusu sukari, baada ya kuwataka kuendelea kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi tofauti na zuio lake la awali.

Waziri huyo alitoa zuio hilo Februari 12 aliposema kuwa Serikali haitatoa vibali kwa wazalishaji wa sukari nchini kwa kuwa kufanya hivyo husababisha wajikite zaidi katika kuagiza badala ya kuzalisha.

Lakini jana alibadilika.

“Kampuni za sukari za TPC, Kilombero, Kagera na Mtibwa zitapewa vibali vya kuagiza sukari kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya tani 215,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa mwaka,” aliwaambia waandishi wa habari jana.

Alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya Serikali kufanya tathmini na kuridhishwa na mipango mikakati iliyowekwa na kampuni hizo za kuongeza uzalishaji wa sukari hadi kufikia tani 345,000 kwa mwaka.

Sukari ilipanda bei kwa kasi mwaka 2016 baada ya Serikali kutangaza bei elekezi ya bidhaa hiyo.

Lakini Serikali ilisema kasi hiyo ya kupanda kwa bei ya sukari ilitokana na wafanyabiashara kuificha na hivyo kuanza msako katika maghala, hali iliyosababisha bidhaa hiyo kuendelea kupanda bei.

Tanzania kwa sasa inazalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka, wakati mahitaji ni tani 670,000 kwa mwaka.

Na tani 515,000 zinatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku tani 155,000 zinatumika viwandani.

Hasunga pia alisema ni matumaini yake kukamilika kwa miradi mingine ya kuzalisha sukari kama wa Bakhresa Group, kutasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji sukari nchini.

Mradi huo uliopo Bagamoyo unatarajiwa kuzalisha tani 100,000 za sukari kwa mwaka baada ya kukamilika ifikapo mwaka 2021, alisema Waziri Hasunga.

Hasunga alisema mpaka kufikia Februari 15, akiba ya sukari ilikuwa tani 129,228 wakati mahitaji kamili ni tani 38,000 kwa mwezi.

Pia Waziri Hasunga alisema miradi mingine ya sukari inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.