Zitto aweka msimamo wa ACT Maalim Seif akitua Zanzibar

Kiongozi wa ACT–Wazalendo, Zitto Kabwe (kulia) na Maalim Seif Sharif Hamad wakiwa wamevishwa mataji ya maua baada ya kuwasili mjini Unguja, Zanzibar jana. Picha na Mtandao

Unguja/Dar. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema uamuzi wa Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na chama hicho ni mwanzo wa mapambano ya kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kupata haki zao.

Wakati Zitto akitoa kauli hiyo visiwani Zanzibar jana, jijini Dar es Salaam viongozi wa Jumuiya ya Baraza la Vijana wa CUF (Juvicuf) walitangaza kujiunga na ACT kuungana na Maalim Seif.

Maalim Seif alijiunga na ACT Machi 18, sambamba na viongozi wakuu wa zamani wa CUF na jana alikaribishwa katika ofisi za CUF za Vuga mjini Unguja ambazo zimegeuzwa kuwa za chama chake hicho kipya.

Huku akitolea mfano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Zitto alisema upande wa Zanzibar umekuwa ukikosa haki za kisheria kwa muda mrefu kutokana na utawala uliopo kutokuwa na nia nzuri na vyama vya upinzani.

Alisema wananchi wa Zanzibar sasa wanapaswa kutambua kuwa mwanzo wa kupatikana kwa haki zao kupitia ulingo wa siasa umewadia kwa kuwa ACT imeandaa mipango imara, ambayo hata hivyo hakuielezea kwa kina.

Alisema mipango hiyo haina maana kuwa chama hicho kina ugomvi na Serikali, bali lengo lake ni kupata haki ya kufanya siasa, kutetea wananchi, kukosoa na kupongeza pale itakapohitajika.

“Huu si wakati wa kuanza mapambano na Serikali kwa mambo yasiyo na msingi. Huu ni wakati wa kuanza mapambano mapya ambayo pia yatatufanya tupate wanachama wapya,” alisema Zitto.

“Hivi sasa wananchi wanataka siasa za kuona upatikanaji huduma bora za kiuchumi, afya na hayo ndio malengo yetu. Tutafanya ziara Pemba na Unguja kwa siku nne (kuanzia leo) lengo ni kuzungumza na wanachama wapya na kutoa kadi. “Niwaombe wananchi msichokozeke au kwenda kinyume na sheria ili malengo yetu ya kusonga mbele kisiasa yaweze kutimia. Sisi tunasema Shusha Tanga Pandisha Tanga.”

Jijini Dar es Salaam waliokuwa viongozi waandamizi wa Juvicuf, walitangaza kuhamia ACT kwa maelezo kuwa wanataka kuunganisha nguvu na kuimarisha upinzani.

Miongoni wa viongozi hao ni Aisha Said aliyekuwa makamu wa mwenyekiti wa Juvicuf, Anderson Ndambo (mkurugenzi wa mipango na uchaguzi) na Abeid Khamis Bakari (mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma).