‘Zitto feki’ amuibua Bashe, adai atawataja wabaya wake

Muktasari:

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amewajibu wanaomhusisha na kuhama chama hicho akisema bado yupo ndani ya chama hicho tawala na kusisitiza siku akitaka kuondoka hatojifichaficha

Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema ipo siku atawataja wabaya wake ambao wanataka kumfanya aone Chama cha Mapinduzi (CCM) sio chama sahihi kwake huku akisisitiza bado yupo sana ndani ya chama hicho tawala nchini Tanzania.

Jana, katika Mtandao wa Twitter kuliibuka taharuki baada ya ukurasa wa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kuonekana ukitoa baadhi ya matamko ambayo baadaye yalikanushwa na viongozi wa ACT-Wazalendo pamoja na Zitto mwenyewe.

Katika jumbe hizo ambazo baadaye zilibainika sio matamko ya Zitto Kabwe zilimtaja Bashe na Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye zikiwahusisha na wao kujiunga na chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo.

“Hili Genge la kihuni ambalo linaongozwa na wahuni wachache ipo siku nitawataja kwa majina ila mpango wenu wakutaka kunifanya nione CCM si chama sahihi kwa Mimi kuwatumikia wananchi wa Nzega na Tanzania HAUTAFANIKIWA, CCM bado nipo sanaaaaaa, shindaneni na mm kwa hoja na si vioja” aliandika Bashe katika akaunti yake ya Twitter

Ujumbe huo aliuambatanisha na picha mbalimbali za matamko hayo ‘feki’ akisema siku akiamua kuondoka ndani ya CCM hatafanya kwa kificho kwani wanaomfahamu huwa hafanyi mambo kwa kujificha.

“Wanaofahamu siasa za Tanzania na za Vyama na wanaonifahamu vizuri misimamo ama maamuzi yangu ya kisiasa huwa sifanyi kwa njia za kificho ama za kichimvi, siku nikiamua kuondoka CCM nitaondoka hadharani ,sitasubiri njia za kificho ama za Kichimvi kama hizi mnazo OTA,” aliandika Bashe

Jana Zitto  alisema tayari amewasiliana na mamlaka kuhusiana na suala hilo na akaunti yake ya Twitter imesimamishwa hadi hapo baadaye.