1,216 wapoteza maisha ajalini

Wednesday April 24 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu matukio 2,593 ya ajali za barabarani yamesababisha vifo 1,216 ikilinganishwa na vifo 1,985 vilivyotokea kipindi kama hicho mwaka  2017/18.

Akisoma bajeti ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2019/2020 leo Jumatano Aprili 24 bungeni jijini Dodoma, waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola amesema vifo 769 vimepungua sawa na asilimia 38.7.

Amesema mwaka 2017/18 matukio ya ajali yalikuwa  4,180 ikilinganishwa na ya 2018/19 hivyo kuwa pungufu ya 1,587 sawa na asilimia 38.

“Vilevile idadi ya majeruhi imepungua kwa asilimia 40.7 kutoka majeruhi 4,447 mwaka 2017/18 hadi majeruhi 2,639 mwaka 2018/19,” amesema Lugola.

Amesema kupungua kwa ajali na vifo kumetokana na usimamizi mzuri wa sheria za usalama barabarani, ushirikiano wa wadau sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzingatia utii wa sheria.

“Katika kudhibiti ajali za barabarani jeshi la polisi limefanya ukaguzi kwa mabasi 247,514 na mabasi 26,219 yaligundulika kuwa mabovu.”

“Mabasi hayo hayakuruhusiwa kuendelea na safari na wamiliki wake walitakiwa kuyatengeneza. Madereva 72 wa mabasi ya abiria walifungiwa leseni zao baada ya kufikishwa mahakamani,” amesema  Lugola.

Amesema katika kipindi hicho madereva 7,271 walifikishwa mahakamani wakiwamo 1,436 wa magari, 5,835 wa bodaboda, huku wengine 95,081 wakipewa adhabu ya kulipa faini kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Advertisement