1,637 waajiriwa Zanzibar mwaka 2017/18

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi Gavu

Muktasari:

  • Watumishi 1,637 wameajiriwa katika wizara na taasisi mbalimbali za  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2017/2018

Unguja. Watumishi 1,637 wameajiriwa katika wizara na taasisi mbalimbali za  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwaka 2017/2018.

Kauli hiyo imetolewa  leo Jumatatu Mei 20, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi Gavu kwa niaba ya waziri wa Wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo mwaka 2019/2020.

Amesema wafanyakazi hao wamepatikana  baada ya kutolewa tangazo la kazi na  Tume ya Utumishi Zanzibar kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Amesema tume hiyo imewaongezea muda wa utumishi serikalini wafanyakazi  14, kubadilisha kada watumishi 49 na kuwapandisha daraja watumishi 11, na kwamba ajira 20 za mkataba zimeidhinishwa huku watumishi  saba wakipewa likizo bila malipo.

Amebainisha kuwa tume hiyo pia imetoa vibali vya kustaafu kazi kwa hiari kwa watumishi 25, kustaafu kazi kwa kufikia umri wa lazima kwa watumishi 563, na 32 kustaafu kazi kwa maradhi.