12 waliotaka kumrithi Lissu waingia mitini, mgombea CCM akosa mpinzani

Muktasari:

Mgombea ubunge wa CCM Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ndio pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kati ya wagombea 13 waliojitokeza

 


Singida. Mgombea ubunge wa CCM Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ndio pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kati ya wagombea 13 waliojitokeza.

Mtaturu amerejesha fomu hiyo leo Alhamisi Julai 18, 2019  kabla ya saa 10:00 jioni, muda ambao wagombea wote waliochukua fomu walitakiwa kuwa wamezirejesha.

Wagombea wengine waliochukua fomu ni  Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK), Amina Ramadhan (DP) na Ayuni John (UDP).

Wengine ni Amina Mcheka (AAF), Maulid Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Ikungi, Thomas Mwailafu akizungumza na Mwananchi amesema hadi muda wa mwisho wa uchukuaji na urejeshaji fomu unamalizika, ni Mtaturu pekee ndio aliyerejesha fomu.

Uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Julai 31, 2019 kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu aliyepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na utoro bungeni.

Tayari Mwailafu amebandika fomu ya Mtaturu katika mbao za matangazo wa ofisi ya halmashauri ya Ikungi ili kutoa fursa ya watoa pingamizi hadi kesho Ijumaa  saa 10 jioni.

Mwailafu amesema kama hakutakuwa na pingamizi lolote  atamkabidhi cheti cha ubunge wa jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Lissu tangu mwaka 2010 hadi Juni 28, 2019.

Lissu yupo nje  Tanzania tangu Septemba 7, 2017 akitibu majeraha ya risasi 16  alizomiminiwa akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea.