Ajali ilivyokatisha maisha ya Sharo Milionea

Tuesday November 27 2012Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27)

Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27) 

By Waandishi Wetu

TASNIA ya sanaa ya hasa ya uigizaji, imekumbwa na giza lingine baada ya mmoja wa waigizaji mashuhuri, Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27) kufariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia jana.

Gari la mwigizaji hiyo lilipoteza mwelekeo na kupinduka mara kadhaa wakati akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda kijijini kwao, Lusanga mkoani Tanga, na kusababisha kifo chake saa 2.30 juzi usiku.

Mwandishi wa gazeti hili alifika nyumbani kwa wazazi wa msanii huyo jana na kupokewa na vilio vya waombolezaji.

“Masikini mdogo wangu, ametutoka akiwa mdogo, masikini mama yetu, ndoto za kujengewa nyumba na kuboreshewa maisha zimeishia barabarani,” ni maneno aliyokuwa akiyatoa dada wa marehemu.

Dada huyo aitwaye Rehema Kadiri (38) alilieleza Mwananchi kuwa msanii huyo alikuwa akienda kijijini, Lusanga kumpelekea mama yake mzazi fedha kwa ajili ya kulimia shamba.

Alisema ahadi hiyo alikuwa ameitoa wiki iliyopita alipokuwa amekwenda kijijini hapo kuhudhuria kumbukumbu ya marehemu babu yake, Mkieta Juma aliyefariki dunia mwaka juzi.

Mazingira ya ajali

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongiji cha Songa Kibaoni, Kijiji cha Songa, wilayani Muheza, Abdi Zawadi alisema ilipofika saa 2.30 usiku wakazi wa eneo hilo walisikia kishindo kikubwa ndipo wakaenda kushuhudia.

Alisema walipofika eneo la tukio, walikuta gari aina ya Harrier likiwa limepinduka, huku mwili wa mwanaume mmoja ukiwa pembeni, ndipo walipomfuata na kumkuta ameshakufa.

“Tulimtambua kuwa ni Sharomilionea baada ya kupekuwa mfukoni na kukuta kitambulisho cha mpiga kura kikiwa na jina la Hussein Ramadhani kikionyesha kuwa alijindikisha Lusanga, tukapaiga simu Kituo cha Polisi Muheza na askari wakaja kuuchukua mwili.

Mwananchi ilipofia eneo la tukio ilishuhudia mti mkubwa aina ya mjohoro uliogongwa baada ya gari hilo kuachia njia, ukiwa umeanguka na gari kupinduka hadi umbali wa mita kama 50.

Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema ndani ya gari hilo lalikuwamo dereva peke yake, likiendeshwa kwa mwendo mkali, na baada ya kupinduka dereva huyo ambaye ndiye msanii Sharomilionea alitupwa nje.

“Hata kama angekuwa amefunga mkanda, kiukweli kwa jinsi gari hilo lilivyogonga mti mkubwa vile na kuuangusha, lazima angekatika kwani katupwa mbali sana,” alisema Bakari Hassan.

Kauli ya polisi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Songa Kibaoni, Wilaya ya Muheza na Sharomilionea (sasa marehemu) ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo.

Umati hospitalini

Katika Hospitali Teule wilayani Muheza, umati wa wananchi ulifurika baada ya kusikia aliyefariki katika ajali hiyo alikuwa msanii huyo.

Katika mji wa Muheza na vitongoji vyake wananchi walimiminika hospitalini hapo wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Muheza, Herbert Mntangi na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu kushuhudia hali hiyo.

Mntangi alilazimika kufanya kazi ya ziada ya kuwasihi wananchi waliokusanyika chumba cha maiti wakiwa na shauku ya kuingia ndani kuushuhudia mwili wa msanii huyo.

“Jamani naomba fanyeni subira, subirini wataalamu wafanye uchunguzi kwanza, lakini pia inabidi uandaliwe utaratibu maalumu wa namna ya kuushuhudia mwili.

“Hivi mnavyofanya vurugu siyo ustaarabu,” alisema Mntangi, na baada ya kauli yake ndipo wananchi wakaachia lango la chumba cha maiti.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Julius Mgema alisema polisi ndiyo walioufikisha mwili wa marehemu hospitalini hapo saa 3 usiku na wakaupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya taratibu nyingine.

Familia ilivyopokea taarifa

Kwa upande wake, Mtoto wa Mama Mdogo wa Msanii huyo, Emmanuel Paulo alisema wao kama familia wamepokea kwa masikitiko msiba huo na pengo lake halitaweza kuzibika kutokana na mchango wake katika familia yao.

“Tuna masikitiko makubwa kutokana na msiba wa ndugu yetu, najua tunaumia ila kazi ya Mungu haina makosa,” alisisitiza ndugu huyo huku alibubujika machozi katika eneo la Hospitali ya Teule wilayani Muheza.

Aliongeza kuwa ndugu yao huyo alitokea Dar es Salaam hadi Kata ya Hale wilayani Korogwe juzi akitumia gari yake binafsi, kwa mujibu wa taarifa ambazo zilitolewa na rafiki yake wa karibu.

Kwa mujibu wa Paulo, kutoka Hale kwenda Muheza, Msanii huyo aliazima gari la rafiki yake, nalilopata nalo ajali.

“Yule rafiki yake aliyeazimwa gari, alimwambia Sharomilionea kuwa gari ambayo anaiazima sio yake, bali ni ya mama yake.”

Wasanii wamlilia

Wasanii mbalimbali wamesema ni kipindi kigumu kwao baada ya kuondokewa na wasanii wawili katika kipindi kifupi, akiwemo Mlopelo aliyefariki Jumamosi wiki iliyopita, na jana wamemzika msanii mwingine wa Bongo Movie, John Stephano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasanii hao walionyesha kushtushwa na kifo cha Sharo Milionea ambaye kwa siku za karibuni alivuta mashabiki wengi kutokana na filamu za vichekesho.

Rafiki mkubwa wa marehemu Sharo Milionea, Mussa Kitale ‘Kitale’ alisema: “Siamini kama Sharo amefariki, nilikuwa nampigia simu ilikuwa inaita muda mrefu bila kupokewa na baadaye usiku Tundaman akanipigia kunipa taarifa za kifo, sikuamini.

“Mzee Majuto naye akanipigia, na mjomba wa Sharo naye alinipigia, nikaamini japo sikuamini na mpaka sasa sitaki kuamini kama Sharo sitamuona tena.”

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba alisema: “Ni pigo kubwa katika tasnia ya filamu, vijana wanazidi kupuputika tena nyota zao zikiwa zinang’aa.

“Sharo amezimika kama mshumaa kwenye upepo mkali, hatuna jinsi zaidi ya kumuombea na kuiombea familia yake, siku zote tunasema kazi ya Mungu haina makosa.”

Steve Nyerere alisema: “Tunamalizia msiba wa Stephano leo (jana) mimi ndio mwenyekiti wa kamati ya mazishi, kisha saa 10 (jana) tunaelekea Tanga kumzika kipenzi chetu Sharo, ambaye naweza kusema amefariki akiwa ameanza kupata mafanikio, alianza kupata matumaini. Ni sawa na unatupa mbegu halafu hujui kama itachipua au itaozea ardhini.

“Sharo alianza kuchipua, ameanza kujitegemea yeye kama yeye, sababu katika maisha lazima uanze wewe, pili uiangalie jamii inahitaji nini kwako.

“Alijitahidi, amejipatia usafiri maskini ya Mungu, kapata pa kulala, katoka Dar kwenda Tanga kuwaona wazazi kwa gharama zake mauti yamemkuta. Jambo la msingi tumuachie Mungu na kuondoa mawazo mabaya kuhusu na kifo chake.”

Filamu alizoshiriki

Sharo Milionea aliibuka katika filamu mbalimbali akiigiza na King Majuto, ikiwemo ‘Mtoto wa Mama’ Back From New York, Kitale na Sharo ambayo ni tangazo ambalo limeingizwa kwenye milio ya simu.

Msanii huyo alipata umaarufu zaidi katika matangazo yake ya Airtel Money akiwa na King Majuto pamoja na lile la Azam Cola hasa staili yake ya kuongea ‘Kisharobalo’ akitumia maneno kama ‘Haaa! nimebugi meeeen! Ooooooh Mamaaa.

Akimzungumzia msanii huyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Mallya alisema tasnia ya sanaa imepoteza mtu muhimu kwani ndiyo alikuwa anaanza kuja juu.

“Tunasikitika kama Watanzania wengine, hasa washabiki wake, alikuwa mcheshi, mtu wa utani na masihara...sisi kama Airtel tutashiriki kikamilifu katika mazishi yake,” alisema Mallya ambaye hata hivyo alisita kusema kama watasitisha urushaji matangazo yake au la

Advertisement