ZUHURA YUNUS: Haikuwa ndoto yangu kuwa mtangazaji

Saturday January 24 2015

Mtangazaji wa BBC Idhaa ya Kiswahili ambaye

Mtangazaji wa BBC Idhaa ya Kiswahili ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza kutangaza kipindi cha Dira ya Dunia, Zuhura Yunus. Picha na Said Khamis 

By Goodluck Eliona, Mwananchi

Dar es Salaam. Siyo jambo la ajabu kwa wasikilizaji wa redio au televisheni kuiga sauti za watangazaji kutokana na umahiri wanaouonyesha wawapo kazini.

Pia, ni jambo la kawaida kwa watangazaji kuwa wanaiga magwiji waliokuwa wakiwasikia kabla ya kuanza kazi ya utangazaji.

Hata hivyo, siyo watangazaji wote walipokuwa watoto walikuwa na ndoto ya kufanya kazi hiyo. Mmoja wao ni Zuhura Yunus, ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa masuala ya wanyama na mimea.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha Dira ya Dunia cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), anasema tangu kuzaliwa kwake alitamani kuwa daktari na siyo vinginevyo.

Akizungumza katika ofisi za Mwananchi jana, Zuhura anasema ndoto ya udaktari ilikufa baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya wanyama na mimea katika Chuo Kikuu cha Mbale kilichopo Uganda.

“Baada ya kuhitimu masomo nilianza kutafuta kazi ndipo kaka yangu aliniambia kuwa Redio Times wametangaza kazi niende nikajaribu,” anasema Zuhura kuwa huo ndiyo ulikuwa mlango wake kuingia kwenye tasnia ya habari.

Hata hivyo, anasema alipokuwa Shule ya Sekondari ya Weruweru aliyosoma kati ya mwaka 1990 hadi 1994, alikuwa akichaguliwa na kusoma taarifa ya habari kila siku asubuhi mbele ya wanafunzi wenzake.

“Kulikuwa na redio ndogo nasikiliza halafu nakwenda kwenye mkusanyiko wa wanafunzi, nasimama na kusoma habari. Natamani ningekumbuka ni nani alinichagua kusudi nimuulize kwa nini alinichagua mimi,” anasema.

Zuhura, ambaye ni mwanamke wa kwanza kutangaza kipindi cha televisheni cha BBC cha Dira ya Dunia, anasema alipokuwa shuleni alitamani kufanya kila kitu.

“Halafu ilikuwa kama unasoma habari haufanyi kazi ngumu, nikasema hapo ndio safi na nikakubali,” anasema.

Pamoja na hayo yote hakufikiria kuwa utangazaji upo kwenye damu, bali aliendelea kusoma masomo ya sayansi akiwa kidato cha tano na sita.

“Ningejua mapema, ile ilikuwa ndiyo alama yangu. Ningeachana na sayansi nichukue masomo mengine, lakini nilisoma masomo ya PCB (fizikia, kemia na baiolojia),” anasema Zuhura ambaye sasa ana shahada ya uzamili ya awasiliano ya umma.

Hata alipokwenda Uganda kwa ajili ya shahada ya kwanza ya wanyama na mimea, hakuwa na wazo la kuingia kwenye uandishi wa habari.

Alivyopata kazi redioni

Zuhura anasema aliporudi nchini mwaka 2000, wakati akijiandaa kupata kazi na kuwa daktari, ndipo kaka yake alimtaka ajaribu kuomba kazi Kituo cha Radio Times. “Wakati naenda kufanya usaili nilishangaa kuambiwa niende, wakati najua mimi sikusomea uandishi wa habari,” anaeleza.

Anasema anadhani kaka yake alimwambia aende kufanya kazi ya utangazaji kwa kuwa anajua kuwa anapenda muziki.

“Bahati nzuri nilipokwenda nilipata kazi. Nilikuwa na wenzangu Soggy Doggy Hunter, Jamila Kilahama, Rahabu Fungo, Taji (Liundi) alikuwa bosi wetu,” anasema.

Siku ya kwanza studio

“Nakumbuka walinipa mwongozo wa kipindi wa kusoma ulikuwa na majina ya Kichina, ambayo nilisoma vizur,” anasema na kuongeza kuwa woga ulimsumbua siku za mwanzoni.

“Nakumbuka mara ya kwanza Taji alinipa habari akaniambia twende studio na akawasha kinasa sauti, mimi sina habari. Akaniambia soma, nilipomaliza aliambia ‘ulikuwa live’, nilishtuka.

“Akaniambaia kama ningekwambia kabla usingefanya ulivyofanya. Aliniambia umefanya vizuri sana, ndiyo alivyonisaidia,” anasema.

Anasema akiwa Redio Times alitangaza kipindi cha asubuhi cha Sunrise cha Kiingereza, Independent Woman cha kila Jumamosi na kipindi cha muziki cha Zee A Cruise.

Zuhura anasema watu wengi wanamfahamu kwa jina la Zee A (Zuhura Abdallah) alilolitumia akiwa Redio Times.

Anapoulizwa iwapo anajuta kupoteza muda kusomea fani ya udaktari bila kuifanyia kazi, Zuhura anasema: “Sijutii uamuzi niliouchukua kwa kuwa ninaamini elimu niliyonayo imenisaidia katika kazi ninayoifanya sasa.”

“Naweza kuwa sijatumia taaluma yangu moja kwa moja, lakini wakati mwingine unaweza kufanya mahojiano ya kisayansi, kidogo inanikumbusha,” anasema.

Zuhuru anasema japokuwa aliipenda Redio Times, mwaka 2003 alihama na kujiunga na Redio Uhuru FM kwa sababu alitaka kukua zaidi kitaaluma.

Anaeleza kuwa watangazaji wa Radio Uhuru FM, Aboubakar Liongo, Masoud Masoud na Sebastian Maganga walikuwa wakivutiwa na utangaziji wake hasa katika kipindi cha Zee A kilichokuwa kikipiga nyimbo za zamani.

“Walikuwa wanasema huyu ni nani, labda atakuwa mtu mzima fulani, kuja kuniona wakasema kumbe mtu mwenyewe ndio huyu. Unajua wakongwe wakikusikiliza halafu wanakukubali unasema ‘waoo’,” anasema.

Ajiunga Mwananchi

Kutokana na mabadiliko ya umiliki wa Radio Uhuru FM, Agosti 2004 aliacha kazi hiyo na kujiunga na magazeti ya Mwananchi na The Citizen.

Zuhura anasema kwa kuwa tangu alipojiunga na tasnia ya habari alikuwa akifanya kazi redioni, ilikuwa vigumu kwake kuanza kuandika habari magazetini.

“Mtu ambaye ametoka redio ukimpa gazeti umemwambia kitu kigumu sana. Mimi niliambiwa niende The Citizen na wengine wakapewa Mwananchi,” anasema.

Hakumbuki habari ya kwanza aliyoiandika alipoingia Mwananchi ilihusu nini, lakini anachokumbuka ni kuwa alipoliona kwa mara ya kwanza jina lake kwenye The Citizen alifurahi.

“Wakati naanza nilikuwa upande wa habari pekee, lakini baadaye kwa jitihada zangu mwenyewe nilianza kuandika makala.

“Nilipenda makala kwa sababu kulikuwa na uhuru zaidi wa kiuandishi kuliko kwenye habari. Nilikuwa naandikia The Citizen lakini nikaanza kuzipeleka na Mwananchi,” anasema.

Anasema wahariri wengi walimsaidia ‘kunoa’ uwezo wake wa kuandika habari, lakini hawezi kumsahau David Mbulumi na Sakina Datoo aliyemsaidia bila yeye kujua.

“Sakina alikuwa ananipa stori karibu kila Jumapili. Ukiangalia stori kubwa utaona jina langu. Nilikuwa nachekelea mpaka basi,” anasema huku akicheka na kuongeza kuwa kwa jambo hilo, akimwona Sakina lazima amshukuru.

Anasema habari anayoikumbuka zaidi ni ile aliyoiandika akiwa Makete mkoani Iringa kuhusu watoto yatima waliokuwa wakiishi mazingira magumu. Ili kuwasaidia watoto hao, ulianzishwa mradi uitwao Mama Mkubwa.

“Kila mtoto alikuwa anachagua mama yeyote kijijini kwa sababu walikuwa wanaamini kwamba watoto walikuwa wanakuwa karibu na ndugu wa upande wa mama zao,” anasema.

“Kila mtoto alikuwa anasema ni mama mkubwa gani anampenda, lakini huyo mama mwenyewe naye hali yake ilikuwa taabani, ilikuwa inasikitisha sana. Tulikuwa waandishi wengi kutoka vyombo vingine, lakini kutoka Mwananchi nilikuwa mimi,” anasema.

Itaendelea kesho.

Advertisement