Mahakama yautaka upande wa mashtaka kukamilisha utetezi wa Kitilya na wenzake

Mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Hurry Kitilya (kulia) na wenzake, Sioi Solomon na Shose Sinare wakiwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha  aliyaeleza hayo  baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi  kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Kamishna Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry  Kitilya na wenzake wawili kukamilisha upelelezi kwa wakati.

Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha  aliyaeleza hayo  baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi  kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Mutalemwa aliieleza mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwaambia kuwa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bado wanaendelea kuwafanyia uchunguzi washtakiwa hao na akaomba kesi ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo na Mutalemwa, Wakili wa Kujitegemea, Alex Mgongolwa anayewatetea washtakiwa hao alihoji mbona mahakama inapelekwa gizani kwa kuwa kila kesi inapofika mahakamani upande wa mashtaka unasema upelelezi bado haujakamilia.

Mgongolwa alidai wateja wake sasa wana miezi sita wapo rumande na wanateseka hivyo aliiomba mahakama iwaeleze upande wa mashtaka waeleze upelelezi umefikia katika hatua gani.

Hakimu Mkeha baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka na utetezi, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati na akaiahirisha kesi hadi Novemba 4, 2016 kwa ajili ya kutajwa