Tuielewe dhana ya diplomasia ya uchumi

Muktasari:

Kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na Serikali ni diplomasia ya uchumi. Wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi wanategemewa kufanya kazi ya diplomasia ya uchumi pamoja na mambo mengine.



Kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na Serikali ni diplomasia ya uchumi. Wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi wanategemewa kufanya kazi ya diplomasia ya uchumi pamoja na mambo mengine.

Kwa mantiki hiyo, utendaji wao utapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hiyo. Ipo mitizamo mbalimbali kuhusu dhana ya diplomasia ya uchumi kama inavyojadiliwa katika makala haya.

Diplomasia ya uchumi

Wawakilishi wa Tanzania nchi za nje wakiwamo mabalozi hufanya shughuli nyingi za kuiwakilisha nchi.

Shughuli hizo ni za kisiasa, kijamii, kijeshi, kibiashara na kiuchumi pamoja na mengineyo.

Dhana ya diplomasia ya uchumi inaweza kumaanisha uwakilishi wa nchi nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi.

Mambo haya ni pamoja na yale yahusuyo uwekezaji na biashara. Kila moja kati ya haya ni muhimu kwa nchi yoyote inayojihusisha kiuchumi na mataifa mengine.

Kuna mambo ya msingi ambayo lazima yaeleweke vizuri na yazingatiwe ili diplomasia ya uchumi ifanikiwe.

Kuvutia Uwekezaji

Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali.

Ili kuvutia uwekezaji kunahitaji ujuzi maalumu. Pia, lazima kujua fursa na miradi ya uwekezaji iliyopo katika nchi.

Fursa na miradi hii inaweza kuwa katika maeneo kadhaa ya kijiografia kama vile mikoa na wilaya.

Ni lazima kujua malengo makuu, sera na mipango ya nchi katika muktadha wa uwekezaji.

Vilevile ni lazima kujua taratibu zinazotakiwa kufuatwa na mwekezaji katika ujumla wake na katika sekta na mradi mmoja mmoja.

Ni muhimu kujua vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na nchi na namna ya kuvipata.

Ni vizuri pia kutia nguvu za kutosha katika kubakiza wawekezaji baada ya kuwavutia. Ni lazima wanaotekeleza diplomasia ya uchumi kujua yote haya na zaidi namna ya kuyatekeleza inavyotakiwa.

Biashara

Pamoja na kuiwakilisha nchi katika shughuli za uchumi, diplomasia ya uchumi inahusu shughuli za biashara pia.

Yapo mambo mbalimbali yahusuyo diplomasia ya uchumi katika tasnia ya biashara. Kati ya mambo hayo ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kufanya biashara na nchi za nje kwa urahisi.

Mambo haya ni pamoja na kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika.

Diplomasia ya uchumi katika eneo hili, pamoja na mambo mengine, inapaswa kuwezesha wafanyabiashara kupata masoko ya huduma na bidhaa wanazozalisha na kutaka kuuza katika masoko ya nje. Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.

Pamoja na kuwezesha uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, diplomasia ya uchumi inapaswa kuwezesha ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nchi za nje kuja Tanzania.

Hii ni pamoja na kubaini bidhaa na huduma hizi, bei zake na taratibu za kuzinunua ili kuziuza au kutumia Tanzania. Pamoja na hili, diplomasia ya uchumi inapaswa kulenga katika kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara ndani ya nchi walizopo.

Vilevile wanapaswa kusababisha wafanyabiashara kutoka katika nchi walizopo kuhudhuria katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara ndani ya Tanzania. Haya ni pamoja na maonyesho kama ya Saba Saba na Nane Nane.

Utalii

Katika tasnia ya diplomasia ya uchumi, shughuli za kuvutia watalii kutoka nje ya nchi kuingia nchini zinapaswa kuwemo.

Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu walio nje ya nchi wanapaswa kuwa wawezeshaji katika kuletwa watalii nchini.

Kwa mantiki iliyotumika katika uwekezaji na biashara, lazima wajue mambo yote muhimu kuhusu utalii nchini. Haya ni pamoja na vivutio vya aina zote vya utalii vilivyopo nchini.

Ni lazima pia waweze kutangaza na kujibu maswali ya wanaotaka kutalii Tanzania kuhusu namna ya kufika nchini kiujumla na katika kila kivutio cha utalii kimahususi.

Ujuzi wa wanadiplomasia

Kusudi diplomasia ya uchumi ifanyike vizuri, kwa ufasaha, ufanisi na jinsi inavyotakiwa, ujuzi wa wanadiplomasia ni muhimu sana. Hii ni kweli kwa mwanadiplomasia mkuu kama vile balozi na timu yake yote. Kimsingi, diplomasia ya uchumi ni juu ya uchumi kuliko diplomasia pekee. Kwa mantiki hii ni lazima wanadiplomasia wafahamu vizuri na kuwa na weledi kuhusu si tu diplomasia bali zaidi kuhusu uchumi. Hata kama uchumi si kitu ambacho baadhi ya wanadiplomasia wanakifahamu vizuri zaidi, ni ujuzi wa lazima katika kazi ya diplomasia ya uchumi. Uzuri ni kuwa kila mara kuna nafasi ya kujifunza kile tusichofahamu kama nchi na zaidi sana kama mtu mmojammoja wakiwemo wanadiplomasia.