Ugonjwa wa homa ya mapafu waongoza kwa vifo 2018

Muktasari:

  • Serikali imesema katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018 homa ya mapafu imeongoza kwa kusababisha vifo, ambapo kwa mwaka 2017, homa hiyo imechangia asilimia 18.2 ya vifo vyote na mwaka 2018 imechangia kwa asilimia 12.9 ya vifo vyote.

Dodoma. Ugonjwa wa homa ya mapafu umetajwa kuongoza kwa asilimia 12.9 ya vifo kati ya magonjwa 10 yaliyochangia vifo mwaka 2018 ambapo watu 2,590 walifariki kwa ugonjwa huo.

Takwimu hizo zilizokusanywa na DHIS2 zimeainisha ugonjwa wa shinikizo la damu ukiwa na kiwango kidogo cha asilimia 1.9 cha watu waliofariki katika kipindi hicho.

Hayo yamezungumzwa leo Ijumaa Januari 18,2019 mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akitoa  taarifa ya hali ya huduma za afya katika kipindi cha mwaka 2018.

Waziri Ummy amesema kiwango cha vifo vya homa ya mapafu kimepungua ikilinganishwa na asilimia 18.2 ya vifo katika kipindi cha mwaka 2017.

Amesema ugonjwa wa shinikizo la damu umeingia kwenye orodha ya magonjwa 10 ambayo yalisababisha vifo kwa mwaka huo.

“Ugonjwa wa shinikizo la damu haukuwa kwenye orodha ya magonjwa 10 yaliyosababisha vifo kwa mwaka 2017 lakini kwa mwaka 2018 umeingia kwenye orodha hiyo na kusababisha vifo 382 hivyo jitihada zinahitajika katika hilo,” amesema.

Magonjwa mengine ni kukosa pumzi watoto vifo 1,269, ugonjwa wa moyo 1253, kifo cha mtoto tumboni kuchubuka ngozi 766, malaria 693, Ukimwi 605, kifo cha mtoto ngozi haijachubuka 540, magonjwa mengine 538, maambukizi katika damu kwa watoto 496.

Ummy amesema katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza wanatarajia kuanzisha mpango wa kupambana na magonjwa hayo ambapo wataanza na ugonjwa shinikizo la damu, kisukari, saratani pamoja na magonjwa ya moyo.