Waziri Mwinyi: Tudumishe amani na kuvumiliana

Muktasari:

Leo Jumapili imefanyika hafla ya Mazazi ya Mtume Muhammad iliyofanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi alikuwa mgeni rasmi na amewataka kudumisha ushirikiano baina ya taasisi zote za dini

Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi ametoa rai kwa taasisi zote za kidini nchini kuvumiliana na kustahimiliana pale panapotokea tofauti ili kusaidia kulinda amani iliyopo.

Waziri Mwinyi ameyasema hayo leo Jumapili Januari 20, 2019 wakati akitoa hotuba katika hafla ya Mazazi ya Mtume Muhammad iliyofanyika mtaa wa Indira Ghandi na kuandaliwa na Nida Textile Mills(T) Limited.

“Kwanza nawafikishia salamu za kheri kutoka kwa Rais John Magufuli na makamu wa rais Samia Suluhu Hassan ambao wanawatakiwa maadhimisho mema na kusisitiza  muendelee kuonesha upendo umoja na mshikamano," amesema Waziri Mwinyi ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa .

Amesema siku hiyo ya Maulid ni siku ya kipekee ambayo imeendelea kukumbusha kuhusu harakati za Mtume Muhammad na kwamba Waislam wote hawana budi kumuenzi kwa kuhuisha umoja, mshikamano na undugu miongoni mwao.

Amewasisitizia Waislam kuimarisha amani duniani kote ni wajibu wa kila mmoja wetu na kwamba ndiyo msingi wa kila binadamu kuishi maisha mazuri na kila mmoja kuabudu kwa imani yake.

"Mtume alihimiza kuwa mtu yeyote hawezi kuwa bora zaidi ya mwingine kwa sababu ya rangi yake ama kabila lake ila kitu pekee kitakachompa daraja hilo ni kutenda haki na kumuogopa Mungu kuwa na ushirikiano katika nyanja zote." Amesema.

Waziri Mwinyi pia amewaombea wale waliopoteza maisha katika tukio la kigaidi lililotokea nchini Kenya, Mungu awalaze mali pema na awaponye waliopata majeraha pia awaepushe na majanga kama hayo na hapa kwetu ayafukuzilie mbali majanga hayo.