Jaji Mihayo ‘ampiga shule’ Waziri Kigwangalla

Muktasari:

Siku mbili baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kuivunja Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kile alichodai kushindwa kutekeleza jukumu lake la kukisimamia chombo hicho chenye wajibu wa kutangaza vivutio vya utalii, mwenyekiti wa bodi hiyo Jaji mstaafu Thomas Mihayo amefunguka kuhusu sakata hilo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji mstaafu Thomas Mihayo, amejitokeza kuzungumzia uamuzi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kuivunja bodi ya wakurugenzi akisema haukuwa sahihi kwani waziri huyo tangu ateuliwe hakuwahi kukutana nayo na kuzungumza ikiwamo kupanga mikakati mbalimbali.

Jaji Mihayo ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 20,2019 kwenye mahojiano maalum na Mwananchi, kuhusu mtazamo wake baada ya bodi aliyokuwa akiiongoza yenye wajumbe sita kutenguliwa na kubaki yeye peke yake.

Amesisitiza ndani ya nafsi yake ana imani kwamba bodi haijafanya mambo ambayo yangemsababishia waziri kuchukua hatua aliyoichukua.

“Kwa sababu tuna uhakika wa dhati kabisa kwamba tangu Waziri wa sasa mheshimiwa Kigwangalla ateuliwe kuwa waziri wa maliasili na utalii, hajawahi kuiita bodi hii kuipa maagizo, hajawahi kuiandikia bodi hii kuipa maagizo wala hajawahi kunipigia simu mimi mwenyekiti wa bodi kunielekeza mambo yoyote,” amesema Jaji Mihayo.

Katika mahojiano hayo, Jaji Mihayo amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo uvunjaji wa sheria uliofanywa na Waziri Kigwangalla, mafanikio waliyoyafanya tangu walipoteuliwa Aprili mwaka 2016. Kujua kwa undani zaidi, fuatilia kesho Gazeti la Mwananchi.