VIDEO: Jaji Mihayo amgeuzia kibao Waziri Kigwangalla

Muktasari:

Siku mbili baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kuivunja Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kile alichodai kushindwa kutekeleza jukumu lake la kukisimamia chombo hicho chenye wajibu wa kutangaza vivutio vya utalii, mwenyekiti wa bodi hiyo Jaji mstaafu Thomas Mihayo amefunguka kuhusu sakata hilo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Thomas Mihayo amepinga uamuzi uliofanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla wa kuvunja bodi ya wakurugenzi.

Jaji Mihayo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wastaafu, ametoa kauli hiyo jana alipozungumza na Mwananchi, ikiwa ni siku mbili tangu Waziri Kigwangalla atangaze kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo Januari 18.

Waziri Kigwangalla alisema wakati akitangaza uamuzi huo kuwa bodi imeshindwa kutekeleza maelekezo yake yenye lengo la kutangaza vivutio vya utalii, lakini hakumgusa mwenyekiti huyo kwa kuwa mamlaka ya uteuzi wake ni Rais.

Bodi hiyo ilianza kazi Aprili 24, 2016 na ilitarajia kumaliza muda wake Aprili 23. Wajumbe wake ni Ibrahimu Mussa, Balozi Joseph Sokoine, Mark Leveri, Richard Rugimbana , Zubein Muhaji Mhita na Augustine Kungu .

Hata hivyo, Jaji Mihayo aliiambia Mwananchi ofisini kwake jana kuwa pamoja na mambo mengine, bodi imekuwa ikifanya shughuli za kutangaza utalii na kwamba imefanya mabadiliko mengi kwa hiyo kuivunja ni kutowatendea haki wajumbe.

Jaji Mihayo alisema ndani ya nafsi yake ana imani bodi haijafanya mambo ambayo yangemsababishia Waziri Kigwangalla kutengua uteuzi wa wajumbe.

Alisema tangu ateuliwe, Kigwangalla hajawahi kukutana na wajumbe wa bodi hiyo.

“Hajawahi kuiandikia bodi hii kuipa maagizo, wala hajawahi kunipigia simu mimi mwenyekiti wa bodi kunielekeza mambo yoyote,” alisema Jaji Mihayo.

“Sasa hatujajua ni mambo gani tumekosea na sisi ni binadamu tunaweza tukakosea. Sisi si malaika lakini kwa dhati yetu tunadhani hatukustahili kwa yote yaliyotokea,” alisema.

Alisema tangu kuhitimu kwake shahada ya sheria mwaka 1972, kuanzia hapo amejihusisha na mambo ya sheria na alipanda ngazi mpaka kufikia Mahakama Kuu.

“Mambo ambayo Mahakama wamezoea kujifunza ni kwamba ukipata kesi yoyote ile imeletwa mbele yako, kitu cha kwanza ukiangalie ni je una mamlaka ya kuisikiliza hiyo kesi?” alisema.

“Kwa maana kuna kesi nyingine inaweza kuletwa mahakama ya wilaya lakini hakimu yule hana mamlaka. Ni kesi ya Mahakama Kuu au madai makubwa kiasi ambacho yapo juu ya uwezo wake,” alifafanua.

Alisema katika utawala bora ni vizuri kabla ya kutoa maamuzi mtu ajiridhishe kama ana uwezo na mamlaka ya kutoa uamuzi.

“Sheria iliyoanzisha bodi hii ni 364 ya mwaka 2002 na katika kiambatanisho chake ambayo imetengenezwa chini ya kifungu cha tatu (2) katika hiyo sheria kinasema, sheria hiyo ndiyo itasimamia mwenendo na jinsi bodi hii ya wakurugenzi ilivyoanzishwa,” alisema.

Alisema kifungu cha kwanza kinasema, “bodi ni mwenyekiti na wajumbe wengine wasiozidi watano”. Kisha inasema “Rais ataianzisha bodi kwa kumteua mwenyekiti na wajumbe wengine watateuliwa na waziri”.

Alisema haiwezekani wajumbe wateuliwe kabla ya mwenyekiti.

Jaji Mihayo alisema mwenyekiti na wajumbe ndio wanaunda bodi.

“Sasa hiyo ina maana kwamba waziri anateua wajumbe wa bodi, lakini anafanya kazi hiyo kwa niaba ya aliyemteua ambaye ni Rais,” alisema jaji huyo mstaafu.

Alisema waziri hawezi kumteua mwenyekiti wa bodi, kwa hiyo hawezi akatengua uteuzi wa mwenyekiti.

“Hiyo ina maana kwamba kisheria waziri hana mamlaka ya kuvunja bodi kwa maana unapoivunja bodi kila kitu kinatoweka, lakini kama sehemu inabaki, basi hujaivunja bodi ndiyo maana mimi bado ni mwenyekiti wa bodi ambaye hata hivyo sina wajumbe,” alisema.

“Nitangojea waziri kuteua wajumbe wa bodi niendelee na kazi labda kabla ya pale niwe nimeondolewa na mamlaka iliyoniteua. Sasa waziri anapowaondoa wajumbe wa bodi ana mamlaka nao, lakini ukiwaondoa wajumbe wa bodi na mwenyekiti anabaki ni kama hujafanya kitu cha ujumla wake.”

Alisema kwa maana hiyo Waziri Kigwangalla atangojea Rais amuondoe mwenyekiti ndiyo neno kuvunja bodi litumike, vinginevyo haliwezi kutimia kwa sababu sehemu moja ya bodi bado ipo.

“Mtu ambaye anaweza akavunja bodi moja kwa moja ni Rais peke yake kwa kuwa amemteua mwenyekiti na wajumbe wengine wanateuliwa na waziri aliyempa mamlaka ya kufanya hivyo. Mtu anayekupa madaraka anaweza kukuondolea wakati wowote,” alisema Jaji Mihayo.