24 waacha shule kwa mimba-Kilosa

Muktasari:

  • Tatizo la mimba ni kati ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na kwamba, wanatekeleza mkakati wa kupambana nazo.

Kilosa. Wakati harakati za kupambana na tatizo la mimba nchini likipamba moto, wanafunzi 24 wa shule za Sekondari katika wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro wamekatisha masomo yao kati ya mwezi Januari na Septemba mwaka huu kwa sababu ya mimba.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Elimu wa Sekondari Wilayani humo, Paula Nkane alisema tatizo la mimba ni kati ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na kwamba, wanatekeleza mkakati wa kupambana nazo.

“Tuna wanafunzi wa kike 7,617  na waliopata ni idadi hiyo niliyoitaja, Serikali inawashughulikia wanaume waliohusika kwa mujibu wa sheria na mkakati wetu ni kusiwe na mwanafunzi hata mmoja atakayeacha shule eti kwa sababu ya mimba,” alisisitiza.

Aliwataka wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza na watoto wao kuhusu miili yao na namna ilivyo hatari kujiingiza kwenye mahusiano wakati wakiwa na umri mdogo.

“Tumeanzisha klabu za wanafunzi kujadili masuala yanayohusu masuala hayo ya afya ya uzazi, wakielewa itakuwa sio rahisi kuanza wakati wakijua bado ni watoto,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mazinyungu Ngamba Manegese alisema katika kudhibiti tatizo la mimba wamekuwa wakiwapima wanafunzi wa kike mara kwa mara.

“Huwa tunawapima ghafla kwa kuwashtukika kila baada ya muda mfupi ili waogope kabisa kujihusisha kwenye vitendo hivyo, akipatikana mwanafunzi mjamzito basi huwa tunamfungulia kadi kabisa ili asije kutoa kabla hatujaanza hatua nyingine,” alisema Manegese.

Hata hivyo alisema maajabu ni kwamba baadhi ya wazazi wakiambiwa watoto wao wajawazito huwa hawastuki kwa sababu ya elimu bure wanaona, hawakuwagharamia chochote jambo ambalo ni tatizo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Zombe wilayani Kilosa, Ismail Kindaile alisema kitakachosaidia kukomesha tatizo hilo wilayani humo ni elimu kwa watoto hasa kuhusu masuala ya afya ya uzazi.

Hata hivyo alisema amekuwa akishirikiana na uongozi wa shule zilizo kwenye kata yake kupambana na tatizo hilo ikiwamo kuwachukulia hatua kali za kishetia wanaume wanaobainika kuwapatia mimba wanafunzi.

Alisema changamoto kubwa iliyopo ni ushirikiano mdogo baina ya wazazi na Serikali hasa kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya familia huwa zinaamua kumalizana kisiri wakigundua vijana wao wamepeana mimba.