Majibu sita ya Magufuli kwa viongozi wa dini

Rais John Magufuli


Muktasari:

Ni baada ya mkutano wake na viongozi hao uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, ambapo walimtajia mambo mbalimbali yanayowakwaza pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali ya maisha na shughuli zao


Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana kwa mara ya kwanza alikutana na viongozi wa dini na kujibu maombi yao waliyowasilisha kwake likiwamo la wananchi kuachwa wazungumze kwa kuwa hiyo ndio demokrasia.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, viongozi hao walimuuliza pia kuhusu masuala ya uwekezaji, kamari, ajira, kilimo cha korosho, mabadiliko ya tarehe ya uchaguzi, maji, elimu ya dini pamoja na kilimo.

Katika majibu yake, Rais Magufuli alimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuyatafutia ufumbuzi baadhi ya masuala yaliyoelezwa na viongozi hao wa kiroho huku mengine akiyatolea majibu.

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Rais Magufuli aliwataka viongozi hao kusema ukweli na kutoa changamoto wanazoziona ili zifanyiwe kazi kwa sababu wao wanawakilisha kundi kubwa la jamii ya Watanzania.

“Leo ni siku ya kwanza kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali kukaa kwa pamoja Ikulu hivyo nitapenda kusikiliza kutoka kwenu na nitazungumza machache baadaye kama yatakuwapo,” alisema.

Maswali na majibu

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lymo alimuomba Rais Magufuli kuwaachia uhuru wananchi wa kuzungumza pale inapowezekana kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.

“Kwa kazi unayoifanya, watu hawatachagua maneno, bali watachagua kazi kwa hiyo kama kuna uwezekano waachie pumzi kidogo wazungumze lakini hawatakushinda kwa maneno yao,” alisema Lyimo.

Akijibu hoja hiyo, Rais Magufuli alisema kiongozi yeyote anaruhusiwa kuzungumza ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ndani ya majimbo yao kwa kufuata taratibu za kupata kibali kutoka polisi.

Alisema sababu ya kuzuiwa kufanya mikutano katika majimbo ya watu wengine ni kwa sababu za kiusalama hasa matumizi ya lugha za matusi.

“Nataka kuwahakikishia viongozi wa dini hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mkutano halali mahali alipo na bahati nzuri kwa mujibu wa sheria wanaotoa vibali ni polisi ukienda utapewa,” alisema.

“Wamefanya Dar es Salaam hapa sitaki kueleza yaliyotokea maana yapo mahakamani, wamefanya chaguzi zao ni mikutano, kwa hiyo nataka kukuhakikishia baba Mchungaji Lyimo hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano.”

Alisema anachotaka ni kuona vyama vinaiga mfano ya viongozi wa dini wanavyoheshimiana na kusaidiana kwa sababu ya umoja wao.

“Kama ni mbunge wa Ubungo afanye mkutano muda wote hakuna anayemzuia kwa sababu yeye ndiyo anawaongoza, mheshimiwa (Saed) Kubenea (mbunge wa Ubungo-Chadema) afanye hata siku nzima kwa sababu mimi naamini hiyo ndiyo demokrasia nzuri inayotakiwa,” alisema.

Kiongozi wa Maimamu Jimbo la Chalinze, Alhaj Hamisi Nassor alisema maji yamekuwa ni tatizo kubwa Chalinze jambo ambalo linafanya baadhi ya watu kushindwa kufanya ibada misikitini.

Alisema licha ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuambiwa kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka jana tatizo hilo lingekuwa historia, badala yake limeongezeka.

“Mbunge analia, mkuu wa wilaya, mkoa wanalia maji, waziri mkuu analia, vilio hivi vimetoka huko chini hadi kufika huku juu. Hebu fikiria ule mradi wa Wami ni jipu basi watumwe watu ionekane pale kuna tatizo gani ambalo linafanya mradi usikamilike maji yawafikie watu,” alisema.

“Hadi tunanunua ndege tumefika mbali sana, sasa kwa nini pale Chalinze maji yasipatikane?”

Akijibu swali hilo, Rais Magufuli alisema makandarasi wamekula karibu fedha zote za mradi wa Chalinze na kwamba ili kumfukuza ni lazima atafute fedha za kutangaza upya mradi huo.

“Unajua ukikuta chungu kimeharibika kukifinyanga kikae sawa unachukua muda, huo ndio ukweli lakini nataka nieleze mradi wa Chalinze ni muhimu na ndio maana aliyekuwa waziri wa Maji hatukumpa mradi mwingine na aliyekuwa katibu mkuu hayupo kwa sababu wao ndiyo chanzo cha kuharibu mradi wa Chalinze na Lindi.”

Makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora Tanzania, Zainuddin Adamjee alisema miongoni mwa mambo yanayozungumzwa hivi sasa ni kamari kusema kauli ya Hapa Kazi Tu kwa kampuni za kamari imekuwa “hapa kamari tu.”

Kama ilivyokuwa korosho, kuhusu kamari Rais pia alimuagiza Waziri Mkuu Majaliwa kulifanyia kazi suala hilo kwa sababu linajenga tabia ya kutofanya kazi huku akitolea mfano kuwa katika nchi nyingine, mambo ya kamari hayatangazwi.

Askofu wa Kanisa la Biblia, John Mchopa alisema ana shaka na watu wanaofanya uhakiki wa korosho huku akibainisha kuwa anahisi kuna baadhi ya wakulima wataumizwa na suala hilo.

Alisema licha ya kuwa uamuzi uliochukuliwa na Serikali kununua korosho ni mzuri, uhakiki huo unafanyika taratibu mno na kuwafanya wananchi waendelee kuteseka.

“Kwa mfano, kanisa dogo la kijijini lina mikorosho yake michache sasa kwa sababu halina akaunti wakaamua kutumia ya mshirika mmoja na limekuwa tatizo mpaka leo hawajapata pesa zao,” alisema Mchopa.

“Sio kwamba wale wa kangomba peke yao tu ndiyo hawajalipwa, bali wapo baadhi ambao wana kilo 100 hawajapata malipo yao.”

Katika majibu yake katika hilo, Rais Magufuli aliwaagiza watendaji husika kuhakikisha malipo hayo yanafanyika huku akimuagiza Waziri Mkuu kusimamia.

“Kamati za uhakiki za korosho wasaini document (nyaraka) za watu wasikae wanawachelewesha watu kulipwa wakati pesa zipo, nataka wakulima wa korosho walipwe pesa mapema na fedha zipo.”

Kuhusu elimu na afya, Rais Magufuli alisema, “Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika utoaji wa huduma hizo hayo mengine ni changamoto na tutazishughulikia. Katika afya Serikali imesaini mikataba na hospitali 92 za taasisi za dini kwa ajili ya kuwapatia vifaa tiba.”

Kuhusu misamaha ya kodi, alisema taasisi za dini zinapostahili kupewa misamaha ya kodi zitapewa na mwaka 2016, zilisamehewa Sh19.66 bilioni, mwaka 2017 ilikuwa Sh17.6 bilioni na mwaka 2018 msamaha ulikuwa Sh46.84 bilioni.

Kuhusu mavazi yasiyo ya staha, Rais Magufuli alisema, “Tusaidiane katika kuhakikisha watu hawa kuheshimu maeneo mengine kama wanavyovaa nguo za heshima kanisani basi wafanye hivyo sehemu nyingine.”

Maombi mengine

Viongozi hao pia waligusia suala la kilimo cha umwagiliaji, ajira kwa vijana na kuwasilisha ombi la watendaji serikalini kujenga utamaduni wa kukutana na viongozi wa dini jambo ambalo Magufuli aliliridhia.

Viongozi hao pia walizungumzia suala la viongozi kuwaweka ndani watendaji mbalimbali.