Alichokisema Mwijage baada ya kutimua mbio bungeni

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage akikimbia kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge baada ya King'ola kulia bungeni leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Shughuli za Bunge zilizokuwa zikiendelea kwa kipindi cha maswali na majibu jijini Dodoma leo Jumanne Februari 5, 2019 ziliahirishwa kwa muda baada ya king’ora kulia wakati kikao kikiendelea


Dar es Salaam. Kama unafuatilia mkutano wa Bunge jijini Dodoma hakika unajua kilichotokea katika kikao cha leo Jumanne Februari 5, 2019.

Wakati kikao hicho kikiendelea kilisikika king’ora na baadhi ya wabunge kuanza kutimua mbio wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge kabla ya baadaye kurejea tena ukumbini, kutolewa hofu na Spika Job Ndugai.

Miongoni mwa walioonekana kuwa na kasi ya kukimbia ni mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ambaye pamoja na mambo mengine amelieleza Mwananchi kuhusu kasi yake hiyo ya kukimbia.

“Mimi ni mtaalamu wa fani ya usalama kwa maana ya safety na nimeishi na kufanya kazi kwenye mazingira haya kwa miaka,” amesema Mwijage.

“Inapotokea king’ora cha tahadhari unapaswa kutulia na kubaini ni nini kinaendelea. Unapaswa kuangalia njia ya kuondoka kwa kufuata njia iliyo wazi kwenda sehemu salama.”

Waziri huyo wa zamani wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji amesema, “Baada ya kutulia na kuwatuliza wenzangu king’ora kilipoendelea mlango wa kuingia bungeni usawa wa Spika ukafunguka, nikavuta kasi ili nitoke kabla haujafunga.”

Amesisitiza, “Ni kanuni za usalama inapotokea hatari. Kumbuka nimewahi kuwa Senior Safety and Environment Control Officer (Ofisa Mkuu wa Usalama na Mazingira) wa TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli)  nikisimamia miundombinu ya mafuta na gesi ambayo ni hatari.”

Akitoa ushauri kwa matukio kama hayo Mwijage amesema, “Kwanza kanuni za kuitikia tahadhari ya dharura iko chini. Mfano tulipotoka nje (wabunge), watu walikaa mlangoni kabisa, je kama kungekuwa na mlipuko? Sehemu ya kukutana wengi hawakujua ilipo.”

“Inapotokea tahadhari ni kutoka na kama njia ipo wazi unatakiwa kutoka haraka kadri iwezekanavyo. Usihangaike kutafuta begi au vitabu na kwa wadada viatu vya mchuchumio vivuliwe.”

Ameongeza, “Kwa taasisi kama Bunge inapashwa kuendesha mara kwa mara zoezi la kuangalia utayari wa wabunge kuitikia tahadhari ya hatari yoyote kwani binadamu hatuchelewi kusahau.”