20 wapoteza maisha kwa kuliwa na mamba Kibondo

Muktasari:

Watu 20 wamekufa kwa kuliwa na mamba katika mto  Lwegele uliopo kijiji cha Rukoma kata ya Igalula Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka 10

 


Kigoma. Watu 20 wamekufa kwa kuliwa na mamba katika mto  Lwegele uliopo kijiji cha Rukoma kata ya Igalula Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka 10.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Februari 19, 2019 mwenyekiti wa kijiji hicho, Rajabu Ndalah amesema mto huo unatenganisha eneo la makazi na mashamba ya wananchi, kila siku lazima wavuke kwenda katika shughuli zao za kilimo.

Amebainisha kuwa wakulima wanategemea mto Lwegele kwa shughuli zote kama kuchota maji ya kupikia, kunywa na kuoga.

"Kuna watu wanaliwa na mamba wanapokuwa wanavuka mto huo kwenda kwenye mashamba, wengine huliwa wanapokuwa wakichota maji mtoni na kawaida ya mamba ni mwerevu na mjanja sana anajua kuvizia,” amesema Ndalah.

Mkazi wa kijiji hicho, Fabiano Alfred amesema watu wanapoliwa na mamba, baadhi ya maiti huonekana na nyingine hazionekani.

Mariamu Rajabu amesema shemeji yake, Ramadhani Azfa alikufa baada ya kuliw ana mamba wakati akivuka mto huo, kwamba walifanikiwa kupata mwili wake.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Lutobola Weja amekiri kupokea taarifa ya watu kuliwa na mamba, kubainisha kuwa Serikali itajenga daraja la wapita kwa miguu ili kuwawezesha wakulima kwenda kwenye shughuli za kilimo bila kuwa na hofu ya kuliwa na mamba.