Serikali ya Tanzania yakaribisha wafanyabiashara kununua korosho

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema mfanyabiashara, Brian Mutembei wa kampuni Indo Power Solutions ya Kenya anakamilisha taratibu za kisheria na biashara kwa ajili ya kununua tani 100,000 za korosho

Arusha. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema mfanyabiashara, Brian Mutembei wa kampuni Indo Power Solutions ya Kenya anakamilisha taratibu za kisheria na biashara kwa ajili ya kununua tani 100,000 za korosho nchini Tanzania.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 20, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha huku akiwakaribisha wafanyabiashara wengine zaidi kununua korosho kwa kiwango cha chini wanachoweza.

"Hadi jana Februari 19, 2019 Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko chini ya timu ya pamoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo ilikua imekusanya jumla ya tani 221,060 za korosho ghafi kutoka kwa wakulima," amesema Kakunda.

Amesema amepatikana mnunuzi mwingine ambaye ni kampuni ya Bi -Southern ya jijini Dar es Salaam itakayonunua tani 15,000 za korosho baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mkataba  na maelekezo ya kisheria kutekelezwa.

Kakunda ameeleza hayo zikiwa zimepita siku 10 tangu kusambaa kwa taarifa kuwa kampuni ya Indo Power haina uwezo wa kununua tani 100,000 za korosho nchini.

Serikali ikajibu taarifa hiyo kuwa haiangalii mambo mengine, bali uwezo wake wa kutekeleza masharti ya mkataba.

Januari 30, Serikali ilitangaza kumpata mteja atakayenunua tani 100,000 za korosho kwa Dola 180,000 za Marekani (zaidi ya Sh418 bilioni) na wiki mbili tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, gazeti la kila wiki la The East African lilichapisha habari kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa mwaka 2016 haina historia ya kufanya miamala mikubwa kiasi hicho.

Katibu mkuu wa wizara ya viwanda na Biashara, Profesa Joseph Buchweishaija alilieleza Mwananchi kuwa historia si hoja ya msingi waliyoipa kipaumbele.