Masaibu ya wagonjwa katika mfumo wa rufaa Kanda ya Ziwa

Mkuu wa kitengo cha dharura na daktari bingwa wa magonjwa ya dharura kutoka Hospitali ya Bugando, Dk Shahzmah Suleman. Picha na Herieth Makwetta.

Muktasari:

Lucy alijua kuwa amefika hospitalini hapo kwa kuchelewa, huku akikiri kwenda kinyume na maelekezo aliyopewa na madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, ambayo iko umbali wa kilometa 160 kutokea Mwanza.

Mwanza. Alfajiri ya Machi 29, mkazi wa Rorya mkoani Mara, Lucy Manase akijikongoja kwa maumivu, alifika sehemu ya mapokezi katika kitengo cha dharura cha Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) mkoani Mwanza, akisindikizwa na ndugu zake.

Lucy alijua kuwa amefika hospitalini hapo kwa kuchelewa, huku akikiri kwenda kinyume na maelekezo aliyopewa na madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, ambayo iko umbali wa kilometa 160 kutokea Mwanza.

Lakini akielezea masaibu yake, alisema hali hiyo ilitokana na matatizo ya kifedha, “Pia nilidhoofika sana, ningewezaje kufika ndani ya muda niliopangiwa?”

“Tarehe 13 madaktari wa Hospitali ya Misheni ya Mara walinipa barua ya rufaa kuja hapa Bugando,” alisema Lucy huku akionyesha dalili kuwa alikuwa akivuta kumbukumbu ili kubainisha kile kilichomtokea.

“Madaktari waliniambia nina uvimbe kwenye shingo ya kizazi na ninahitajika kupatiwa huduma maalumu hapa Bugando. Lakini nililazimika kusubiri nyumbani kwa siku kadhaa baada ya kupewa barua ya rufaa. Familia yangu ilikuwa ikijaribu kutafuta fedha za kunisaidia,” anasema Lucy ambaye ni mkazi wa Shirati wilayani Rorya.

“Awali nililazwa hospitali ya misheni ya wilayani kwangu, ilikuwa Desemba 23. Nilifanyiwa upasuaji na niliendelea kupatiwa matibabu hadi Desemba 30 mwaka jana. Madaktari walisema ninahitaji huduma ya kitaalamu zaidi,” anasema na kuongeza:

“Ndugu zangu walinileta hapa. Tulifika kwa gari binafsi. Hakukua na gari ya wagonjwa kwa ajili ya kunifikisha hapa,” anafafanua.

Hata hivyo, simulizi ya namna hii haimuhusu Lucy pekee. Yeye ni miongoni mwa wagonjwa wengi ambao wanafika Hospitali ya Bugando kwa kuchelewa pindi wapatiwapo rufaa kwa ajili ya huduma za kitaalamu zaidi.

Utafiti uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa matatizo ya kifedha na usafiri kutoka vijijini kwao hadi kwenye hospitali hiyo ya rufaa ya kikanda iliyopo mjini Mwanza, yanachangia kwa kiwango kikubwa kuchelewa kwao tangu wanapopewa rufaa kutoka kwenye hospitali zilizopo kwenye maeneo yao.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Huduma za Dharura wa Hospitali ya Bugando, Shahzmah Suleman, wagonjwa wengi wanaotoka kwenye vituo vya afya na hospitali za Kanda ya Ziwa bado hawajajua namna mfumo wa rufaa kwa wagonjwa unavyofanya kazi.

“Kuna baadhi ya kesi ambazo wagonjwa wamekuwa wakifurika kwenye vituo vya ngazi za chini vya huduma za afya wakiwa hawajui kuwa matatizo yao yanahitaji kutatuliwa kwenye hospitali za juu hasa ngazi ya rufaa za mkoa au kanda,” anasema wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika hospitalini Bugando.

Dk Suleman anasema mfumo wa utoaji rufaa hufanywa kwa mtindo wa piramidi. Ngazi ya chini kabisa ni zahanati, ikifuatiwa na kituo cha afya, kisha hospitali ya wilaya, mkoa na hospitali za rufaa kikanda na kitaifa. Tatizo linaposhindikana katika ngazi ya chini, linahamishiwa kwenye ngazi ya juu yake.

Anasema changamoto iliyopo ni ya wagonjwa wenyewe na wakati mwingine wahudumu wa afya ambao huchelewa kutoa barua za rufaa kwa wagonjwa.

“Tumekuwa tukisisitiza kwa wafanyakazi wa ngazi za chini kuhakikisha kwamba utaratibu unafuatwa lakini mara nyingi imekuwa vigumu kutekeleza kwa ufanisi,” anasema.

“Lakini pia tumekuwa tukipokea wagonjwa ambao wamekaa nyumbani kwao kwa muda mrefu baada ya kupewa barua za rufaa. Wapo wanaochelewa kwa wiki hadi mwaka, wakiwa na matatizo makubwa na sugu. Wengi hulalamika kuwa matatizo ya kifedha ndicho chanzo,” anasema Dk Suleman na kuongeza:

“Tumeliona hili zaidi kwa watu wanaotoka maeneo ya Mikoa ya Geita, Musoma na Shinyanga,” anasema.

“Wapo wengine ambao hupewa barua za rufaa lakini wanaamua kwenda kwenye tiba za jadi au za kiimani wakiwa na matumaini ya kupona. Hawa huw awanafika hapa wakati hali zao zikiwa mbaya,” anaeleza.

“Wakati wote imekuwa changamoto hasa pale mgonjwa napopewa rufaa kuja hapa akiwa na upungufu wa damu kwa sababu tu imeshindikana kupatikana katika vutuo vya chini. Hii inaonesha kuwa ipo haja ya kuhakikisha kuwa huduma kama hizi zinaboreshwa katika vituo vyetu vya afya,” anasisitiza.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa BMC, Dk Bahati Wajanga anasema idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka Kanda ya Ziwa kwenda Hoapitali ya Taifa ya Muhimbili imekuwa ikipungua sana baada ya hospitali hiyo ya Bugando kuwekeza katika huduma muhimu, ikiwamo ya mionzi ya saratani na upasuaji wa viungo na mifupa.

“Wagonjwa ambao bado tunawapeleka Dar es Salaam ni wale wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo pale kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete,” anafafanua.

“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kwa sasa ni kwamba, hatuna wataalamu wa kutosha katika upasuaji wa viungo na mifupa. Tunaye mmoja tu kwa sasa. Pia tunaye mtaalamu mmoja wa usingizi. “Tuna wajibu wa kuhakikisha mfumo wa rufaa unafanya kazi kwa mujibu wa mahitaji na protokali zake. Njia moja ni kwa kusaidia wafanyakazi wa afya katika vituo vya chini kujenga uwezo wao hasa wa kitaaluma.

Na wataalamu wetu wanaweza kusaidia kwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya zikiwamo za upasuaji. Hii inaweza kusaidia kwa kiasi,” anapendekeza.

Lakini, anafafanua kuwa kuna haja ya kuhakikisha Watanzania wote wanaunganishwa kwenye mfumo wa bima za afya ili kupunguza mzigo wa gharama za malipo ya fedha kwa huduma za afya.

Kwa mujibu wa mkuu wa Huduma za Upasuaji wa BMC, Dk Leonard Washington, ipo haja ya kupitia upya sera ya afya ili kupelekwa wataalamu wengi kwenye hospitali za rufaa za mikoa.

“Huduma maalumu za kiafya kwa wajawazito na watoto wanaozaliwa, upasuaji, wagonjwa ya watoto, huduma za radiolojia na utoaji wa dawa za usingizi ambazo zinahitajika katika ngazi hii,” anasema. Anaamini kwa uimarishaji wa utoaji wa huduma za afya katika ngazi ya hospitali za mikoa na wilaya, itapunguza kiwa kiwango kikubwa idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda hospitali za rufaa za kikanda na za kitaifa, na hivyo kupunguza msongamano katika hospitali hizo.

“Tatizo wanalokumbana nalo wagonjwa wanapopewa rufaa ni pamoja la malazi. Wengi wanalazimika kuishi mbali na jamaa zao. Hii pia ina madhara katika suala zima la uponaji wao,” anasema.

“Wagonjwa wanaofika hapa wakitokea maeneo ya mbali wanahitaji sana uangalizi wa ndugu zao. Hii husaidia hata katika uponaji wa haraka. Lazima tujenge miundombinu yetu ili ndugu na jamaa wa wagonjwa waweze kuwa karibu na wagonjwa wao kwenye hospitali za rufaa,” anasisitiza Dk Washington.

Anasema BMC ina mpango wa kujenga hosteli maalumu kwa ajili ya jamaa za wagonjwa wanaotoka mbali.

Anaamini kuwa hiyo itasaidia sana kwa wagonjwa kupata huduma sahihi za afya na kutunza fedha.

“Hii ina maana kuwa jamaa za wagonjwa hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kutoka kwenye wilaya zao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wao.

Hiyo ina gharama kubwa. Wataweza angalau kutunza fedha ambazo wanatumia kusafiri wakati wote wa kumuhudumia mgonjwa wao. Wataweza kusaidia upatikanaji wa huduma bora za kiafya,” anafafanua Dk Washngton.

Shirika lisilo la Kiserikali la Friends of Children with Cancer Tanzania, limeendelea kusaidia kuwawezesha wagonjwa ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu katika hospitali za rufaa na za Kanda ya Ziwa

Muasisi wake, Walter Miya anasema, “Tumeona baadhi ya wagonjwa wenye saratani wakipewa rufaa kwenda hospitali maalumu lakini wameamua kubaki nyumbani kwa hadi mwaka mzima. Wanapata changamoto sana. Hivyo tumekuwa tukijaribu kukusanya nguvu ili kuwasaidia kupata huduma za afya,” anasema.