Zitto achambua uamuzi wa jaji aliyewapa dhamana Mbowe, Matiko

Muktasari:

Kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo amekubaliana na hoja ya jaji kuwa kufuta dhamana mshtakiwa kunahitaji hoja kubwa zaidi ya kumpa, na kuzitaka mahakama kuzingatia ukubwa wa kosa wakati wa kutoa masharti ya dhamana.


Dar es salaam. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amepongeza uamuzi wa Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu baada ya kufuta uamuzi wa kuwafutia dhamana, viongozi wawili wa Chadema, Freeman Mbowe na Esther Matiko.

Wawili hao walifutiwa dhamana na Mahakama ya Kisutu kwa kukiuka masharti ya dhamana baada ya kutofika mahakamani katika kesi ya jinai inayomkabili Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, Matiko (mbunge wa Tarime Mjini) na viongozi wengine 13.

Wameachiwa leo Alhamisi Machi 7, 2019.

Uamuzi wa Jaji Rumanyika ulimvutia Zitto, ambaye alimpongeza, akisema moja ya sababu za kutenguliwa kwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ni kuwa kesi ya jinai inayowakabili viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, inadhaminika.

Amesema Jaji Rumanyika pia ameeleza kuwa kutoa dhamana ni tafsiri dhahiri ya mahakama ya dhana ya Katiba kuwa mtuhumiwa hawezi kuwa na hana hatia mpaka Mahakama itakapomtia hatiani.

Alisema katika uamuzi huo wa Jaji Rumanyika kumewekwa msingi mwingine kuwa kufuta dhamana kunahitaji sababu kubwa kuliko hoja za kumpa mtu dhamana.

Zitto ameeleza katika uamuzi huo Jaji amezitaka Mahakama kuzingatia ukubwa wa kosa kutoa masharti ya dhamana .

Amesema katika uamuzi huo, jaji ameelekeza masharti ya dhamana yawekwe bila kuweka hisia kuwa mpango ni kunyima mshtakiwa dhamana.

Zitto amesema hoja iliyozungumzwa na jaji ni kuwa mahakama izingatie adhabu kwa makosa yaliyopo mbele yake ili pale ambapo mshatikiwa akitiwa hatiani asiwe ameadhibiwa mara mbili.

Zitto alisema Jaji Rumanyika pia ameeleza sababu za kunyima dhamana ziwe zinakubalika kwa mahakama yeyote duniani.

Amesema jaji ameeleza kuwa mahakama izingatie msongamano uliopo gerezani na hivyo kupima kama kutoa au kufuta dhamana kunachangia au kupunguza msongamano gerezani.

Katika uchambuzi huo, Zitto amesema Jaji amesema mahakama izingatie kuwa uhuru wa mshtakiwa hauna mbadala.

“Jaji Rumanyika si tu amewaachia huru Mbowe na Matiko, bali pia amefuta masharti ya dhamana ya kuripoti polisi kila wiki,” amesema Zitto ambaye pia ni mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

Zitto ampongeza Jaji Rumanyika na kueleza Tanzania bado ina majaji kwa hakika na akamuombea mola ampe maisha marefu.