Makonda aandaa wanasheria kuwasaidia wajane

Thursday April 04 2019
MAKONDA PIC

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wameandaliwa wanasheria maalum watakaopitia kesi za wajane waliodhulumiwa mali baada ya kufiwa na waume zao.

Makonda amesema hayo katika kongamano la wanawake wajane lililofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo, Makonda amesema wazo la kuwakusanya lilitoka kwa wanawake zaidi ya 300 waliofika ofisini kwake kuomba wasaidiwe kutafuta suluhu ya kesi zao.

Amesema tafiti aliyoifanya kupitia kamati maalum aliyoiunda mwaka jana inaonyesha changamoto za wajane ni nyingi na zinahitaji suluhisho.

"Nia hapa ni kuandaa mfumo wa kudumu wa kutatua changamoto ya wanawake hawa wanaolia, wajane wanatamani kujua namna ya kupata haki zao nimekuja kuwafariji," amesema Makonda.

Amesema wajane wengi baada ya kufiwa hawajui namna ya kuendeleza mali za waume zao baada ya urithi.

Advertisement

"Kwa hiyo unakuta hawajui watawatunzaje watoto baada ya hapo ndio maana leo nimewaita tuzungumze," amesema.

Amewataka wajane walio dhulumiwa mali kujaza fomu maalum kuelezea kesi zao na namba zao za simu ili wanasheria waweze kuwasaidia.

"Mfute mjane machozi kwa kuhakikisha anapatiwa haki zake, wapo wanaosema vitu ninavyoanzisha haviishi lakini bora ninayeanzisha," amesema Makonda.

Awali, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Erick Shigongo alisema anapotazama wanawake wajane anajifunza idadi ya wanaume waliopoteza maisha yao.

Aliwataka wanaume kutafakari kwa kina watakapo fariki watawaacha wake zao na watoto katika wakati gani.

"Neno langu kwenu msikate tamaa bado mna uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yenu," alissema.

Amewataka wanawake kuwa makini katika matumizi ya fedha na muda ili kidogo wanachokusanya kiwasaidie.

Advertisement