MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Shahidi atoa kielelezo cha panga mahakamani

Muktasari:

Kesi hiyo namba 48 /2108 ya mauaji ya kukusudia inawakabili watu wa tatu ambao ni Edward Shayo, ambaye ni mmiliki wa shule hiyo, Hamis Chacha (mlinzi wa shule) na Laban Nabiswa ambaye ni mwalimu.Pia inasikilizwa na Jaji Firmin Matogolo. Inadaiwa kuwa wanafunzi huyo aliu-waa Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa mita 300 kutoka eneo la shule.

Moshi. Mpakiaji wa Kiwanda cha Saruji Moshi, Jackson Daudi, ambaye pia aliwahi kuwa mlinzi katika Shule ya Sekondari Scolastica mwaka 2017 ameiomba Mahakama Kuu ipokee panga alilolionyesha mahakamani ili kutoa adhabu kwa mhusika wa mauaji.

Daudi, ambaye ni shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka, aliiambia mahakama hiyo jana kwamba panga alilotumia mhusika wa mauaji ya Humprey Makundi ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, lipokewe na aliyehusika na mauji apewe adhabu na mahakama hiyo.

Mbele ya Jaji Firmin Matogolo, shahidi huyo alitoa ombi hilo wakati akiongozwa na Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali, Joseph Pande alipokuwa akitoa ushahidi.

Alidai kwamba Novemba 18, 2017 saa 2:00 usiku, askari wa Shule ya Scholastica wakiwa wameongozana na Chacha ambaye alikuwa mlinzi wa shule hiyo, walifika chumba cha walinzi. Alidai Chacha aliongozana nao mpaka sehemu panga lilipokuwa limehifadhiwa.

Alidai kuwa askari hao walipokuta panga kwenye chumba cha walinzi, walimuuliza Chacha, “tangu uje hapa hujawahi kutumia panga? Je, panga ni la nani? Chacha akasema panga ni la kwake na baadaye waliondoka na Chacha”.

Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na wakili Pande yalikuwa:

Wakili Pande: Askari wale walipoondoka na Chacha, wewe ulibaki wapi na wao walienda wapi?

Shahidi Daudi: Nilibaki getini na wao waliondoka.

Wakili Pande: Kesho yake tarehe 18/11/2017 kulitokea nini?

Shahidi Daudi: Saa 2:00 usiku niliona gari jeusi aina ya (Toyota Land) Cruiser yenye vioo vyeusi. Nikafungua geti dogo.

Wakili Pande: Ikawaje?

Shahidi Daudi: Niliona wamefungua gari yao wakamtoa Chacha.

Wakili Pande: Nini kiliendelea?

Shahidi Daudi: Chacha aliwaongoza wale askari mpaka sehemu panga lilipokuwa, lilikuwa kwenye kabati.

Wakili Pande: Ilikuwaje sasa

Shahidi Daudi: Walipofika chumba cha mlinzi walimuuliza Chacha panga ni la nani? Akasema panga ni la kwake pamoja na rungu lililokuwa juu ya meza na baadaye wale askari waliondoka na Chacha.

Wakili Pande: Hili panga unataka mahakama hii ifanyeje?

Shahidi Daudi: Naomba mahakama hii itoe adhabu kwa waliotumia panga hili kufanya mauaji.

Jana jioni shahidi wa tisa katika kesi hiyo, Godlisten Tomari ambaye alikuwa akiongozwa na wakili wa Serikali, Lucy Kyusa alidai kuwa akiwa lindoni Hospitali ya Mawenzi, alipigiwa simu na kiongozi wake akimtaka msaada wake.

Alidai kuwa alipofika ofisini kwa kiongozi huyo, aliwakuta askari watatu ambao walikuwa wamebeba maiti kutokea Himo na kumtaka amsaidie kufungua mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti ili wauhifadhi mwili huo ulioletwa usiku ule.

“Niliwauliza huu mwili umetoka wapi? Wakanambia umetokea Himo hivyo kiongozi wangu alinipa funguo kisha nikaongozana na askari wale katika chumba cha kuhifadhia maiti na mwili uliwekwa kwenye beseni la kusafishia miili ya maiti,” alisema.

“Walipoondoka ilibidi nifungue mwili ule ili nijue kwamba ni binadamu au mnyama. Nilipofunua mwili ule ulikua umevaa soksi, bukta na tisheti na mwili ule ulikuwa umeanza kuharibika, hivyo baada ya kuuhifadhi nilirudisha funguo kwa kiongozi wangu nikaendelea na shughuli zangu kama kawaida.”

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unajumuisha wakili Pande akisaidiana na Abdallah Chavula, Omari Kibwana na Lucy Kyusa.

Upande wa utetezi unawakilishwa na David Shilatu, Elikunda Kipoko, Rwakisa Sambo na Patrick Paul.