Wasomi waitahadharisha Tanzania kuhusu mkataba wa EPA

Muktasari:

Wakati Tanzania ikiendelea na msimamo wa kutosaini makubaliano ya  biashara (EPA) biana ya Afrika na Jumuiya ya Ulaya wasomi wamechambua hatua hiyo huku wengi wao wakiona ni sawa kulingana na wakati

Dar es Salaam. Wasomi wamechambua msimamo wa Tanzania ambayo mpaka sasa haijasaini mkataba wa ushirikiano wa biashara (EPA) kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na nchi za Afrika, huku wakishauri yafanyike upya mapitio ya vipengele vyake ili kuangalia kama una manufaa kwa nchi.

 

Jana Jamatatu Aprili 15, 2019 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilifanya mdahalo kuhusu EPA ambapo watu walijadili iwapo Jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kuutaka mpango huo au kufanya majadiliano upya kuhusu baadhi ya vipengele.

 

Mkataba huo ambao utarahisisha biashara kati ya Afrika na Ulaya umechukua muda mrefu kukubalika baadhi ya nchi zikiwamo mbili za Afrika Mashariki (Kenya na Rwanda) zikwia  tayari zimeridhia, lakini kuna mataifa likiwamo Tanzania yamegoma kusaini mkataba huo.

 

"Miongoni mwa athari za baadhi ya nchi kukubali na nyingine kukataa ni kuathirika kwa umoja wa Afrika ambao bara limekuwa likijivunia," amesema Profesa Helmut Asche wa Chuo Kikuu cha Johaness-Guternberg cha nchini Ujerumani.

 

Asche ambaye alikuwa akitoa mhadhara katika mdahalo huo, amesema miongoni mwa manufaa ya mkataba huo ni soko huria la kuuza bidhaa za Afrika- Ulaya bila ushuru mbalimbali lakini athari iliyopo ni kuua viwanda vya ndani  kwa sababu nchi nyingi za Afrika zinategemea mapato ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoingizwa.

Mchumi huyo na mwanasosholojia amesema lengo la Ulaya ni kujihakikishia soko la bidhaa zake Afrika na kujihakikishia malighafi  hususan rasilimali za ardhini kama madini na mambo mengine.

Amesema mkataba huo utaathiri soko la pamoja na kanuni za forodha katika jumuiya kama EAC.

"Nchi nyingi za Afrika sasa zipo katika mpango wa kujiinua kiuchumi mfano Tanzania na Nigeria ambazo mpaka sasa zimekataa wazi kusaini mkataba huo zipo katika mapinduzi ya viwanda na viwanda vyao vinahitaji ulinzi nadhani ndio sababu hawajasaini," amesema Asche.

Ameongeza  kuwa kupitia mkataba huo nchi za Afrika zitaweza kupata bidhaa zinazotola Ulaya kwa bei nafuu, hii itaonekana kwa bidhaa zile ambazo tangu awali zinaagizwa kutoka katika nchi hiyo.

 

Mhadhiri wa siasa UDSM, Profesa Mohabe Nyirabu amesema kuna umuhimu kwa Tanzania kuendelea kukataa kusaini mkataba huo.

 

"Kuna haja ya kufanya mapitio upya kwa kuzingatia sera zetu za ndani ili kama ni kukubali tuzingatie maslahi yetu kwanza," amesema Profesa Nyirabu.

Mhadhiri mwingine Dk Richard Mbunda amesema Ulaya inatumia nguvu kubwa kushawishi mkataba huo ili kutimiza malengo yake ya kuwa na nguvu ya soko ili kushindana na washirika wengine wakubwa wa Afrika ambao ni China, India na Marekani.

"Nguvu yetu ya kuuza bidhaa na ya kwao hailingani hivyo Tanzania na Afrika kwa ujumla watajikuta wao ni wauzaji wa malighafi lakini bidhaa za bara lote zitakuwa zinatokea ulaya, sio mkataba mzuri kwetu hata kidogo kwa kuwa una manufaa kwa ulaya zaidi," amesema Dk Mbunda.