MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Wamarekani wazuiana kuzungumzia muungano - 13

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere alivyofanya safari ya muda mfupi Zanzibar na kufanya maongezi ya faragha na Rais Abeid Amani Karume kisha baadaye kusaini hati za Muungano kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona kwenda Kenya na Uganda kuwataarifu viongozi wa nchi hizo kuhusu muungano.

Ingawa safari za Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Kambona zilikuwa nyingi, alilazimika kurejea Dar es Salaam kabla ya Aprili 25, siku ambayo Bunge la dharura lingefanya kikao mjini Dar es Salaam.

Aliporejea Dar es Salaam Aprili 24 kwa ajili ya kikao cha dharura cha Bunge kilichopangwa kufanyika siku iliyofuata, alikwenda moja kwa moja hadi Ikulu na kuripoti kuwa amemaliza kazi.

Aprili 23, siku moja baada ya Nyerere kutoka Zanzibar, Balozi wa Marekani nchini Tanganyika, William Leonhart alituma ujumbe mwingine kwenda Washington, Marekani akitoa tahadhari.

“Chicomm (Ukomunisti wa Kichina—Chinese Communism) unaounga mkono wapiganaji wa (Abdulrahman) Babu kuhusu Zanzibar unaweza kuanzisha mapigano ili kuzuia kufutwa kwa chama cha Umma Party na wafuasi wake,” alisema katika ujumbe huo.

Pia alitaarifu kuhusu hofu kwamba Urusi inaweza kuvuruga mipango ya Marekani mapema bila kutazamiwa kwa kuwahi kuondoa ujumbe wa wanadiplomasia wa Ujerumani Mashariki kutoka Zanzibar.

Pia katika ujumbe wake, Balozi Leonhart alionyesha kufurahishwa na maendeleo ya mipango ya muungano.

“Maendeleo (ya mipango ya Marekani) huko Zanzibar yanazidi kuzorota, kukiwa na ongezeko la ushawishi mkubwa wa Babu na Chicomms, kumeithibitishia Serikali ya Tanganyika kwamba aina fulani ya muungano au shirikisho na Zanzibar bado ni uchaguzi bora zaidi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa Tanganyika na kupindua mwelekeo thabiti wa Zanzibar kuelekea kwenye udhibiti wa Ukomunisti wa Kichina,” alieleza.

“Kwa kufuata mfano imekubalika kimsingi kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ufanane na ule uhusiano ulioko kati ya HMG (Serikali ya Uingereza) na Ireland ya Kaskazini.

“Mradi haujawa tayari na hatari zinazoweza kujitokeza zinaonekana wazi. Mambo muhimu yanaonekana kuwa (i) Utatuzi wa Kiafrika kwa tatizo la Kiafrika (ii) Utaratibu wa kisiasa ambao kiasili Nyerere ameuzindua (iii) wepesi na usiri ambao umekuwa ukitumiwa katika mradi huu kwa kutumia nafasi ya kutokuwapo kwa Babu na kuzuia kujizatiti zaidi kwa ukomunisti wa Kichina.”

“Siku chache zijazo zitakuwa muhimu sana. Serikali ya Tanganyika inaimarisha vituo vyake vya polisi Zanzibar, lakini silaha walizo nazo hazina uhakika na silaha zilizo na nguvu nyingi zaidi (kuliko zile za polisi wa Nyerere waliokuwa Zanzibar) zinawezekana kwamba ziko mikononi mwa kambi ya Babu.

“Serikali ya Tanganyika inatambua zawadi ya misaada iliyotolewa na Uingereza kutokana na maombi ya viongozi wa Serikali ya Zanzibar walioko Bara, lakini tuna imani kubwa sana kwamba hakutakuwa na mahitaji ya aina hiyo.”

Alisema katika ujumbe huo kuwa wanaelewa kwamba kikosi cha askari chenye kombania kadhaa na ambacho ni sehemu ya brigedi au rejimenti kutoka Nigeria ambacho kwa sasa kiko Dar es Salaam, hakiwezi kutumiwa nje ya Tanganyika kutokana na makubaliano ya Tanganyika na Nigeria.

Alishauri hali ya tahadhari ipendekezwe kwa vikosi vya Marekani na kuwe na majadiliano ya dharura na naibu balozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam kuhusu tukio lolote litakalojitokeza bila kutarajiwa. Alihisi kuwa Waingereza waliokuwa Dar es Salaam hawakuwa wakipewa taarifa za mradi wa muungano.

“Katika kipindi cha sasa ni muhimu mno kuepuka kutoa taarifa yoyote kwa umma na kutajwa kwa maslahi ya Marekani kuepukwe kabisa. Katika mazungumzo na viongozi wa Kiafrika, tunaamini kwamba njia nzuri zaidi ni kuepuka kuhusisha Vita Baridi katika jambo hili, na kusisitiza kwamba hili ni jambo lililoanzishwa na Waafrika na kufanyiwa uamuzi na watu wa Tanganyika na Zanzibar kwa kadiri wanavyohusika,” alisema Leonhart katika ujumbe wake.

Siku hiyo ya Aprili 23, Dean Rusk, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, alituma ujumbe kwa balozi za Marekani mjini Dar es Salaam na Zanzibar.

“Tupe ushauri haraka kama Zanzibar na Tanganyika wana haja ya kupata vifaa vya kudhibiti ghasia, kama vile mabomu ya kutoa machozi, makombora ya kutupwa kwa mkono na barakoa,” alisema.

Naye Balozi Leonhart alituma ujumbe siku hiyo kwenda washington.

“(mkuu wa itifaki, Wynn Jones) Mbwambo amepiga simu na kutoa ombi binafsi kwa Nyerere na Kambona kuwa taarifa zozote kutoka Marekani kuhusu muungano wa serikali ya Tanganyika na Zanzibar ziepukwe kwa hali zozote,” alisema.

“Hali ya mambo kwa siku chache zijazo katika Zanzibar inaweza kuwa ya hatari kabisa na inajulikana wazi kuwa Warusi na Wachina hawatabiriki. Mwambie Nyerere na umsisitizie kwamba tangazo lake lisiende mbali na mipaka ya taarifa tuliyoitoa kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, na aseme kwamba mradi huo utaamuliwa na watu wa Tanganyika na Zanzibar peke yao.”

Itaendelea kesho