Tanzania yakusanya kodi Sh5.5 bilioni kwenye taulo za kike

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji akijibu maswali bungeni katika kikao cha Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kodi hiyo ya Ongezeko la Thamani (VAT) imekusanywa mwaka 2016/17 na 2017/18 kabla ya kufutwa Juni, 2018

Dodoma. Serikali imekusanya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh3bilioni mwaka 2016/17 na Sh2.5bilioni kwa mwaka wa fedha 2017/18 katika bidhaa ya taulo za kike zilizoingizwa nchini pamoja na zilizozalishwa nchini.

Imesema fedha hizo zilikusanywa kabla ya kodi katika taulo hizo kuondolewa Juni, 2018.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 23, 2019 na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza lililoulizwa kwa niaba yake na mbunge wa viti maalum wa chama hicho, Dk Immaculate Swale.

Katika swali la msingi, Peneza alitaka kujua kodi ambayo Serikali ilikusanya kwa miaka hiyo miwili kabla ya kuondolewa kwa kodi hiyo.

Katika swali la nyongeza, Dk Swale amesema licha ya kodi kuondolewa bado bei ya taulo za kike ipo juu na kutaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha bei hiyo inashuka na kuwa nafuu kwa watumiaji.

Katika majibu yake Dk Kijaji amesema soko ni huru na kwa sasa ipo katika mchakato wa kufanya tafiti kuhusu jambo hilo kwa maelezo kuwa kuondolewa kwa kodi hiyo kunawanufaisha zaidi wazalishaji.

“Kuna nchi kama Botswana na Kenya waliondoa kodi lakini walibaini kuwa haikuleta matokeo chanya. Unapoondoa kodi kuna namna wazalishaji wananufaika. Tutajiridhisha katika tafiti tuliyoanza kuifanya na tutakuja na majibu sahihi hapa,” amesema Dk Kijaji.