60 wapoteza maisha Afrika Kusini

Thursday April 25 2019

 

Durban,Afrika Kusini.Maporomoko ya udongo yaliyotokana na mvua kubwa yamesababisha vifo vya watu 60, katika mikoa ya Durban na KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini, maafisa wanasema.

Zaidi ya watu 1,000 wameondoka kutoka makazi yao kwa mujibu wa Rais Cyril Ramaphosa ambaye ametembelea maeneo yaliyoathiriwa.

Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika maeneo ya Kusini na Mashariki ya nchi hiyo siku chache zilizopita.

Mafuriko zaidi na upepo mkali unatarajiwa katika maeneo ya pwani huku onyo likitolewa kuhusu hali mbaya ya hewa.

Mafuriko hayo makubwa yaliharibu biashara na nyumba za watu pamoja na vyuo vikuu viwili huku mamia ya watu wakikimbia nyumba zao.

Rais Ramaphosa alizitembelea familia zilizopoteza ndugu zao katika mafuriko hayo.

Rais aliweka shada la maua katika eneo ambalo watu wanane wallifarika. Pia alionekana akiwasukuma walinzi waliokuwa wakiwazuia watu waliokuwa wakitaka kumuona.

 

"Ni muhimu kuja kuona kile kilichofanyika au kilichotokea na kuomboleza na familia zilizopoteza wapendwa wao katika janga hili. Kupoteza maisha sio jambo rahisi, hasa maafa yakitokea ghafla," alisema Ramaphosa.

Juzi, alitoa taarifa ya kusema kuwa: "Hali hii inatuhitaji sote kuja pamoja kama taifa kufikia jamii zilizoathirika."

Huku hayo yakijiri, Waziri wa Utawala wa Mkoa Nomusa Dube-Ncube aliwaambia maofisa wa Kituo cha Radio cha SAFM kwamba bado wanaendelea kutathmini kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mkasa huo, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Siku zijazo watu watalazimika kuhamishwa kutoka maeneo yaliyoathirika, alisema.

Advertisement