Waathirika wa fidia wamsuburi Rais Magufuli

Muktasari:

Waathirika 205 waliopisha mradi wa kituo cha pamoja cha forodha kati ya Malawi na Tanzania kumpokea Rais John Magufuli kwa mabango kutaka kujua hatima

Mbeya.  Waathirika 205 wa kijiji cha Njisi wilayani Kyela mkoani Mbeya  waliopisha mradi wa kituo cha pamoja cha forodha baina ya nchi ya Malawi na Tanzania, wamesema ujio wa Rais John Magufuli huenda ukawa   neema ya kulipwa fidia zao baada ya  kupisha mradi huo  mwaka 2016.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Aprili 25, 2019 wamesema baada ya Serikali kufanya tathmini eneo hilo na kuwataka wananchi kutoendeleza shughuli zozote za kiuchumi na makazi, jambo ambalo walitii lakini  cha kushangaza mpaka sasa hawajui hatima yao.

Mmoja wa waathirika hao, Neema Lyolo, amesema wanashindwa kuelewa hatima yao na kwamba huenda ujio wa Rais Magufuli ukawa ukombozi wa matumaini mapya ya kupata haki zao na kuona namna ya kuendesha maisha yao.

"Tunaomba rais wa wanyonge atoe neno lake kutusaidia  wanyonge, kwani tuliahidiwa kulipwa ndani ya miezi sita tangu tupishe mradi lakini mpaka sasa ni miaka mitatu  licha ya viongozi wetu kufuatilia na kutopata majibu ya kuridhisha," amesema.

Naye Diblo Boniface amesema wakiwa Watanzania wazalendo katika nchi yao waliona ni vyema kupisha mradi huo kwani utachangia kuwa chachu ya kukua kwa uchumi baina ya nchi hizo mbili na kujipa matumaini ya kulipwa fidia zao kwa wakati, ili kuendeleza biashara zao na kurejesha mikopo waliokopa katika taasisi za fedha.

"Wengi wetu tulikuwa na vibanda vya biashara na makazi  eneo la mradi sasa tulisitishiwa kuendeleza nyumba zinabomoka na kuezuliwa mapaa na mvua zikinyesha ni shida kubwa kwetu sasa ni vyema Serikali ikatulipa fidia," amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao, Kelly Mwandambo, amesema wanaidai Serikali  fidia ya zaidi ya Sh7 bilioni na amefuatilia kwa viongozi wa mkoa na wilaya bila mafanikio.

"Kimsingi tumefuatilia sana tangu mwaka 2016 lakini tunapigwa kalenda, sasa tumeona ujio wa Rais Magufuli huenda ukawa neema kwetu sisi wanyonge," amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwalipa fidia na mradi huo kuanza.