Viongozi wataka uchunguzi kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Chadema

Muktasari:

Wabunge na viongozi mbalimbali wamepaza sauti kuomba kufanyika kwa uchunguzi juu ya saula la kudaiwa kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyangali maarufu Mdude Chadema

Dar es Salaam. Wabunge na viongozi mbalimbali wamepaza sauti kuomba kufanyika kwa uchunguzi juu ya suala la kudaiwa kutekwa na kupatikana kwa mwanachama wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Mdude Nyangali maarufu Mdude Chadema.

Sauti hizo wamezipaza kupitia mitandao yao ya kijamii baada ya Mdude anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Jumamosi iliyopita ya Mei 4, 2019 mjini Vwawa mkoani Songwe.

Wametoa kauli hizo ikiwa zimepita saa chache tangu Mdude kupatikana akiwa ametupwa na watu wasiojulikana jana usiku Jumatano eneo la Inyala, Mbeya Vijijini.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete ameandika: “Hivi ni vitendo vinavyochafua nchi yetu.”

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameongeza: “Ni muda mwafaka sasa kwa vyombo vyetu vya ulinzi kujipanga kupambana na hali hii inayoendelea kuchafua nchi yetu. Pole sana Mdude, Chadema kwa janga hilo. Nikuombee upate nafuu haraka Mungu atakujaalia kheri.”

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter:  “Pamoja na kufurahia ndugu yetu Mdude Nyangali kurudishwa akiwa hai na kumwombea apone, Tusibweteke.

“Tupaze sauti kutaka uchunguzi wa matukio haya ya utekaji. Ni rahisi kujisahau na kujipongeza kwa kelele mtandaoni na baada ya miezi kadhaa atachukuliwa mwingine.”

Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Fatma Karume ameandika kwenye Twitter yake: “It’s not over (sio mwisho). Tunahitaji information (taarifa) ya hawa watu waovu waliomteka Mdude. Tunahitaji kupata information kutoka wananchi. Hawa watekaji ni binadamu na wanaishi mitaani.”

Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki katika ukurasa wake wa Twitter ameandika: “Pole sana Mdude, Chadema Mwenyezi Mungu mwenye utisho wa utukufu, mwenye uhai wa milele atakurejeshea afya yako.”

Mwanachama wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter: “Nimeamka na faraja kufuatia taarifa za kupatikana Mdude Nyagali baada ya kampeni kubwa ya #BringBackMdudeAlive.

“Nimeumizwa na hali yake mbaya inayoashiria mateso aliyopitia. Wito wangu kwa Watanzania sasa ni kuungana kudai uchunguzi huru wa kimataifa ufanyike kuhusu matukio haya!”