Wanawake milioni mbili hujifungua nchini Tanzania, huduma bado changamoto

Thursday May 16 2019

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serika imesema wanawake milioni mbili hujifungua kila mwaka nchini Tanzania ingawa huduma katika makundi maalumu haijawa ya kuridhisha katika maeneo mengi.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustin Ndugulile ameliambia Bunge leo Mei 16,2019 kuwa taarifa zilizopo serikalini ni kuwa idadi hiyo ya wanawake hujifungua kila mwaka huku umri wa kuishi kwa Mtanzania ukifikia miaka 64.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Kaliua (CUF) Magdalena Sakaya ambaye alitaka kujua serikali itatekeleza lini Sera ya Afya ya huduma za Afya bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

Sakaya pia amehoji mwaka 2014 serikali ilianza utaratibu wa kutoa vitambulisho kwa ajili ya matibabu bure akahoji ni wilaya ngapi zimekamilisha kazi hiyo muhimu ili kuokoa maisha ya wazee yanayopotea kwa kukosa huduma.

Naibu Waziri huyo amesema bado kuna changamoto katika utekelezaji wa Sera hiyo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa na idadi ya watu walio katika makundi maalum.

Amesema utekelezaji wa huduma hiyo katika madirisha umekuwa na changamoto kwasababu ni asilimia 40 tu ya halmashauri zote zimeweza kutekeleza agizo hilo.

Advertisement

Advertisement