Mbivu mbichi aliyempiga kikongwe kujulikana kesho mahakamani Ilala

Thursday May 16 2019

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala kesho Ijumaa Mei 17, mwaka huu itatoa hukumu katika kesi ya jinai namba 180/2018, mshtakiwa Neema Athuman (60) anadaiwa kumpiga Amina Abdallah (80).

Katika kesi hiyo, Neema anadaiwa kumpiga ngumi mbili kikongwe huyo maeneo ya Gongolamboto.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi, Catherine Kihoja, baada mashahidi wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao pamoja na upande wa utetezi.

Hukumu hiyo ilipaswa kusomwa Mei 8, mwaka huu lakini ilishindikana kwa sababu Hakimu Kihoja alikuwa hajamaliza kuiandika hivyo itasomwa kesho.  

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka unawakilishwa na Wakili wa Serikali, Grace Lwila.

Akijitetea mahakamani hapo, Neema alieleza kuwa miaka 11 iliyopita bibi huyo alimuuzia eneo huko Gongolamboto ambako amejenga nyumba na anaishi.

Alidai kuwa Februari 23, 2017 ilikuwa siku ya Alhamisi usiku mvua kubwa ilinyesha na   nyumba yake aliona maji yanajaa na walikuta tundu walilotengeneza 2010  kutolea maji limeziba.

"Hivyo nilimwambia mtoto wangu Josephine Kamela (26) akalitoboe lile tundu, akaomba tindo akaichukua na kuanza kulitoboa katika ukuta wa nyumbani yangu," alisema Neema akijitetea.

Aliendelea kueleza kuwa wakati Josephine akiendelea na kazi ile, akatokea Amina na kumvuta.

"Nikamwambia mama mbona unanifanyia hivi, mtoto wangu aliniambia twende polisi nikamweleza hiyo ni kesi ya serikali ya mtaa," alieleza Neema.

Aliongeza kuwa Februari 28, 2017 walikuwa na ugomvi wa mpaka ambao Amina alikwenda kumshtaki hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alimtuma katibu tarafa alishughulikie na walijieleza.

Lakini siku hiyohiyo, alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Stakishari  Machi mosi 2017, alipelekwa Mahakama ya Mwanzo Ukonga na kwamba wakiwa hapo   Amina alianza kupiga kelele, huku akidai kama ni jela yupo tayari.

Neema alidai kuwa kutokana na dharau hiyo alifungwa jela miezi sita katika gereza la Segerea, lakini alikaa miezi miwili akatoka.

Alieleza kuwa alipotoka akaanza kumfuatilia.

Advertisement